Na Matukio Daima App.
MOROGORO.Polisi Mkoani Morogoro inamshikilia mtu aitwaye Dainess Faustine ambaye ni Askari wa Jeshi la Wananchi nchini Tanzania (JWTZ) akituhumiwa kuendesha chombo cha moto (Gari) huku akiwa amelewa.
Hali hiyo inaelezwa kuwa ilimsababishia kugonga na kuharibu miundombinu ya barabara ambapo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama, amethibitisha tukio hilo akisema limetokea mnamo Mei 17 2025 katika Kata ya Bigwa Manispaa ya Morogoro ambapo mtuhumiwa huyo akiwa amelewa aligonga taa za barabarani.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo alikuwa na gari aina ya Nissan yenye namba za usajili T. 560 EDG na baada ya kupimwa alikutwa na kiwango cha ulevi 305.9.
Polisi inasema kiwango hicho cha ulevi kilimsababishia kushindwa kudhibiti gari lake hilo na kugonga miundombinu ya barabara na uharibifu wa taa za barabarani ambapo ametoa wito kwa jamii kwa ujumla kuacha tabia ya kutumia vilevi hasa wakiwa wanaendesha vyombo vya moto.
0 Comments