Kanisa Katoliki nchini Tanzania ni miongoni mwa taasisi zilizo mstari wa mbele katika kuzungumzia masuala ya kiraia, kisiasa na kijamii.
Wakati nyakati zingine jukumu hili hufanywa kupitia mwamvuli rasmi wa Baraza la Maaskofu TEC, nyakati zingine hufanywa na askofu mmoja mmoja kwa nafasi zao za uongozi wa kanisa.
Bila shaka ni sehemu ya sababu kwanini tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima limeibua huzuni na ukosoaji na pia kuhusianishwa na ukosoaji unaofanywa na Kitima na TEC.
"Kitima alikuwa anakosoa wakati wa Magufuli. Hajawahi kukaa kimya akiona UOVU. Wakati wa Magufuli hakuna aliyemgusa. Swali: Mnadhani sasa mapadri watakaa kimya maana mshawatia uwoga? Tanzania ina amka na huzuni leo" ameandika mwanasheria na Mtetezi wa Haki za Binadamu Fatma Karume katika ukurasa wake wa X.
"…kwa kweli walilenga kumdhulumu maisha yake, kwa sababu wamempiga sehemu za kichwa, na walimpiga zaidi ya mara moja kwa nia ya kutaka kumuua au kumjeruhi vibaya… ni shambulio lililofanywa na mtu mwenye ujuzi wa alichokuwa anakifanya… halikuwa shambulio la kihalifu la kawaida," Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Boniface Mwabukusi ameeleza baada ya kumtembelea Padri Kitima hospitalini.
Taarifa ya polisi inasema Padri Kitima alishambuliwa majira ya saa nne usiku wa Jumatano ndani ya eneo zilizopo ofisi za TEC, jijini Dar es Salaam na mtu mmoja anashikiliwa akihusishwa na tukio hilo.
Bila kujali itikadi ya kiongozi aliyepo madarakani, katika kila muhula wa serikali, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limekuwa likitoa misimamo na matamko katika kila tukio au hali ya kisiasa iliyokuwa inaendelea na kuzua gumzo katika jamii. Na kwa sasa, kwa nafasi yake, Padri Kitima amekuwa ndiye sura ya TEC katika matamko hayo.
Tume ya Warioba Iheshimiwe
Mwezi April 2014, kundi la maaskofu 32 wa TEC walitoa waraka maalumu wa Pasaka wakitaka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuhesimu maoni yaliyokuwa yamekusanywa juu ya Katiba Mpya yaheshimiwe.
"Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu Mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano, mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa Tanzania" ulisema waraka huo walioupa jina la Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.
Mwaka mmoja baadae, Machi 2015, Maaskofu wa Katoliki waliungana na maaskofu wa makanisa mengine ya Kikristo, isipokuwa kutoka kanisa la Sabato, kutoa tamko si tu kupinga rasimu lakini kwenda zaidi na kuwataka wananchi waikatae rasimu hiyo.
Katika ujumbe wao wa Kwaresma mnamo Februari 2018, Maaskofu wa Katoliki walitoka hadharani na kukemea ukandamizwaji wa haki mbalimbali za binadamu chini ya Rais John Pombe Magufuli ambaye pia alikuwa ni muumini Mkatoliki wa dhati.
"Vile vile baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa mahakama na bunge kwa njia ya kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya Kikatiba" walisema Maaskofu
Sakata la bandari
Lilipoibuka sakata la bandari ambapo palikuwepo na mivutano ikiwa Tanzania iingie mkataba na kampuni ya Dubai katika uwezekezaji katika bandari ya Dar es Salaam, baraza la Maaskofu liliitaka serikali isikilize sauti za wananchi
"Tukisukumwa na dhamiri iliyo na lengo la kulinda rasilimali, mshikamano, amani, uhuru, na umoja wa kitaifa; tunathubutu kusema kuwa baada ya miaka 63 ya uhuru wa nchi hii, wananchi hawajapenda kuiachia bandari ya Dar es Salaam apewe mwekezaji mmoja aiendeshe kwa vile Watanzania wenyewe wana uzoefu wa kuiendesha," ilisema sehemu ya waraka wa maaskofu walioupa jina la Sauti ya Watu, Sauti ya Mungu.
Lakini Kanisa Katoliki halijaishia katika kukemea maovu pekee bali wakati mwingine limejitokeza na kutoa mchango katika kurekebisha yale waliyoyaona yasiyofaa.
Mwaka jana mwezi Februari Padri Kitima aliliambia gazeti la The Citizen kwamba Kanisa Katoliki limeanzisha programu waliyoiita Mabalozi wa Amani yenye lengo la kuamsha hamasa ya wananchi katika kushiriki shughuli na matukio mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na michakato ya uchaguzi.
Kanisa Katoliki duniani na siasa

Kujihusisha huku kwa kanisa Katoliki Tanzania kunatokana na Hati maalum ya Kichungaji iliyotokana na maazimio ya mkutano mkuu wa maaskofu wa dunia nzima ujulikanao kama Mtaguso wa Pili wa Vatican uliotoa muongozo juu ya uhusiano wa Ufalme wa Mungu na utawala wa watu duniani.
Katika mkutano huo uliofanyika kati ya tarehe 11 Oktoba 1962 na 08 Desemba 1965, maaskofu walitoka na nakala iliyoitwa Hati ya Kichungaji juu ya Kanisa na Ulimwengu inayosisitiza – pamoja na mambo mengine - uundwaji wa misingi ya kisheria na kisiasa ya haki na usawa inayowezesha raia wote kushiriki kikamilifu na kwa uhuru katika kujenga jamii iliyo bora.
Mwezi Novemba mwaka jana, Kanisa Katoliki nchini Kenya lilikataa kupokea sadaka iliyotolewa na Rais wa nchi hiyo William Ruto. Moja ya hoja zilizotolewa katika kukataa sadaka hiyo ni kulinda uhuru wa kanisa na badala yake walimtaka Rais Ruto kushughulikia mambo ya msingi kama kukomesha ufisadi nchini na kutekeleza ahadi zake za kisiasa.
Nchini Jamuhuru ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) Kanisa katoliki limekuwa mstari wa mbele katika masula ya kisiasa na itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa mwaka 2019 Kanisa hilo lilipinga vikali mchakato wa uchaguzi uliomuweka madarakani rais Felix Tshisekedi na kudai kuwa kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura.
Kabla ya uchaguzi huo, kanisa hilo pia lilikuwa ni moja ya taasisi ambazo zilimuwekea shinikizo rais wa zamani wa nchi hiyo Jospeh Kabila kung'atuka madarakani. Hivi sasa, Maaskofu wa Kanisa hilo wanaendesha juhudi za ndani za kutafuta suluhu ya kisiasa baina ya serikali ya nchi hiyo na waasi wa M23.
Marehemu Papa Francis ni kiongozi wa Kanisa Katoliki ambaye aliheshimika kwa kuzungumzia na kukemea mambo mbali mbali ya kiraia, kisiasa na kijamii.
Katika uhai wake, mbali na kuzungumzia mateso ya Wapalestina huko Gaza, Papa Francis alitembela Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sehemu mbili zenye mafarakano ya wenyewe kwa wenyewe, ambapo aliwasihi viongozi wa nchi hizo kusitisha mapigano na kutafuta amani ya kudumu.
Papa Francis pia alikuwa mstari wa mbele katika kulaani vita vinavyoendelea Gaza, na alikuwa mara kwa mara akiwapigia simu makasisi wa Kipalestina waliokwama katika vita hivyo.
Misimamo ya Padri Kitima
Kwa miaka mingi, Padri Kitima amekuwa mstari wa mbele kukemea uvunjifu wa sheria na ukiukwaji wa maadili nchini katika matukio ya kisiasa na kijamii. Kwa upande mwingine, anafahamika pia kwa kuhusika kupatanisha pale mafarakano yanapoibuka lakini pia kusifia mienendo bora inayolenga kujenga nchi.
Tukio la kushambuliwa kwake limekuja mwezi mmoja tu tangu Rais Samia Suluhu Hassan kuwaonya viongozi wa dini dhidi ya kujihusisha na kile alichokiita masuala ya kisiasa
"Dini ibaki kwenye majukumu yake ya msingi ya kulea waumini kiroho na kimaadili kuendana na misingi ya dini zao. Ila kamwe, viongozi wetu wa dini wasidandie ajenda au vishawishi vya kisiasa na kuweza kuvuruga nchi yetu.
Badala yake viriri au majukwaa ya ibada yatumike kwa ibada yasitumike na wanasiasa kufanyia propaganda zao" Alisema Rais Samia Suluhu Hassan mwezi Machi wakati wa Baraza la Idd, jijini Dar es Salaam.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Rais Samia kimetoa tamko la kulaani shambulio dhidi ya Padri Kitima kikitaka uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
Hata hivyo, Padri Kitima amekuwa akisisitiza kwamba viongozi wa dini na makanisa kwa ujumla wanapozungumzia masuala ya kisiasa na kijamii si tu kwamba hawaingilii siasa bali wanatimiza wajibu wao katika jamii.
Akizungumza na shirika la utangazaji la Ujerumani DW Swahili, Padri Kitima alisema kazi ya kanisa ni kukemea uovu.
"Tutakaposema chagua chama hiki na uache chama hiki, hapo ndipo tutakuwa tumeingia kwenye siasa. Lakini tunaposema acha kuiba kura za mwenzako, acha kuiba kura ya raia aliyempigia huyu ihesabu pale pale. Huo ni uovu, ni ushetani, ni dhambi na lazima iachwe."
0 Comments