Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025, baada ya kufanikisha makusanyo ya Shilingi Bilioni 23.02 kufikia mwezi Mei, sawa na asilimia 125 ya lengo la mwaka.
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 18.36, lakini hadi kufikia Machi mwaka huu tayari ilikuwa imetimiza lengo hilo, na sasa imevuka kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa huo, Mjiolojia Lameck Gabote amesema mafanikio hayo yametokana na usimamizi thabiti wa vyanzo mbalimbali vya maduhuli ikiwemo mrabaha, ada na tozo mbalimbali.
“Mwaka ujao wa fedha 2025/2026 tumepangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 24. Tuna imani kubwa kwamba tutafikia na kuvuka lengo hilo. Mkoa wa Dar es Salaam uko ‘active’ kukusanya maduhuli, hatulali,” amesema Gabote kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa licha ya Dar es Salaam kutokuwa na shughuli kubwa za uchimbaji wa madini, imekuwa kitovu muhimu cha biashara ya madini kutokana na uwepo wa Soko la Kimataifa la Madini, bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa ambavyo hurahisisha biashara ya madini ndani na nje ya nchi.
Aidha, Gabote amebainisha kuwa ofisi yake pia inasimamia mgodi mdogo wa dhahabu uliopo kijiji cha Kibindu, Handeni mkoani Tanga, ambao uzalishaji wake ni mdogo – ukitoa wastani wa gramu 12 hadi 25 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa Gabote, mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imejaliwa kuwa na aina mbili za madini: madini ya ujenzi na madini ya viwandani, ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa makusanyo ya maduhuli. Madini haya yamekuwa yakitumika katika miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara ya BRT unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Takwimu hizi zinaonesha ukuaji chanya wa Sekta ya Madini katika maeneo yasiyokuwa ya uchimbaji wa moja kwa moja, na kuonesha umuhimu wa miundombinu ya biashara kama masoko, bandari na viwanja vya ndege katika kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.
0 Comments