Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 120 vya Mkoa wa Singida utakaogharimu Sh.Bilioni 17.39 ambao utanufaisha jumla ya kaya 3,960 za mkoa huo.
Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema hayo leo (Mei 14, 2025) wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya M/s Transpower Limited na Whitecity International Contractor Ltd JV kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha Sh. 17,394,214,690.85 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 120 mkoani Singida na tumefika hapa Singida kuja kumtambulisha mkandarasi na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” amesema Mhandisi Olotu.
Mhandisi Olotu alisema kati ya vitongoji 2,289 vilivyopo mkoani Singida, vitongoji 1,052 vimefikishiwa umeme na kwamba vitongoji 120 vitakavyopata umeme awamu hii vitaongeza idadi ya vitongoji vitakavyokuwa na umeme mkoani humo.
“Kwa mujibu wa mkataba, mradi huu unapaswa kutekelezwa ndani ya miezi 24 lakini mkandarasi ametuahidi na kutuhakikishia kuwa ndani ya kipindi cha miezi 12 atakuwa amekamilisha mradi,” amebainisha Mhandisi Olotu.
Naye Meneja Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena alisisitiza kuwa umeme ni hitaji la muhimu na kwa kutambua hilo Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa.
“Serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya kusambaza umeme kote nchini, wito wetu kwa wananchi ni kuwapa ushirikiano wakandarasi na kuwa walinzi wa miundombinu hii,” alisisitiza Mhandisi Lwena.
Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego alimshukuru Rais Dkt. Samia Skwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi mkoani humo hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa maendeleo ya jamii.
“Ninayo furaha kubwa leo hii kumpokea mkandarasi huyu kwani kama mtakumbuka Serikali iliahidi ifikapo 2025 itakuwa imekamilisha kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania Bara na sasa tumeshuhudia kabla hata ya 2025 vijiji vyote vilikuwa vimefikiwa na umeme na sasa tunatekeleza vitongojini,” amesema Dendego.
Dendego aliipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza miradi yake kwa ufanisi na uwazi na pia alimpongeza mkandarasi kwa ahadi yake aliyoitoa ya kukamilisha mradi huo kwa miezi 12 badala ya 24 kama ilivyo katika mkataba wake.
“Nimefarijika, tumepata mkandarasi mzuri kwani ametuahidi hapa atakamilisha kazi ndani ya miezi 12 nasi tutampatia ushirikiano na tutamsimamia ipasavyo ili ahadi hii ikamilike kwa kupata mradi bora,” amesema.
0 Comments