Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wananchi wa mkoa huo kuzingatia lishe bora kwa watoto wao ili kujenga msingi mzuri wa malezi na makuzi kwa watoto hao na kupambana na utapiamlo.
Andengenye amesema hayo kwenye hafla fupi ya kukabidhi magari mawili kwa ajili ya uratibu wa Shughuli za Lishe kwa sekta ya afya ya ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na Halmashauri ya wilaya Uvinza na kubainisha kuwa jamii bora daima hujengwa na Msingi wa Lishe bora ambayo husababisha uwepo kwa kizazi chenye weledi, uadilifu na Afya bora.
Amesema utekelezaji wa Afua za lishe ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) 2020 hadi 2025 na kwamba matokeo bora ya lishe yanahitaji ufuatiliaji na usimamizi madhubuti ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na serikali yanafikiwa.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema uwepo wa nyenzo hizo utachangia kufikia ufanisi katika malengo ya serikali kwenye utekekezaji wa afua za lishe.
Amesema pamoja na uwepo wa changamoto ya kutoendelea kwa ufadhili wa mradi wa USAID Lishe Project Kigoma, amewataka wataalam kutekeleza afua za lishe kuendana na bajeti za serikali zilizopangwa badala ya kutegemea wafadhili.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk. Damas Kayera amesema kuwa mkoa bado unakabiliwa na changamoto kubwa ya uwepo wa utapiamlo kwa watoto na kwamba kutolewa kwa magari hayo kutasaidia kuongeza nguvu katika kupambana na changamoto hiyo.
Mwisho.
0 Comments