Na Shomari Binda-Tarime
WANANCHI wa jimbo la Tarime mjini wamemtaja mbunge wa jimbo hilo Michael Kembaki kama mbunge wa pekee katika maendeleo ya elimu.
Licha ya wananchi kumtaja mbunge huyo kama wa pekee Chama cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Tarime haikuwa mbali na wananchi hao kwa kudai ametekeleza ilani pasipo shaka.
Hayo wameyasema kwa nyakati tofauti wakati wakipokea madawati yaliyotolewa na mbunge huyo kwaajili ya shule za msingi.
Mmoja wa wananchi hao aliyeshuhudia upokeaji wa madawati hayo Mwita Mniko amesema wamepita wabunge kwenye jimbo la Tarime mjini kwenye sekta ya elimu Kembaki amekuwa suruhisho.
Amesema madawati aliyoyatoa yanakwenda kuwafanya wanafunzi kukaa mahala sahihi pa kuwawezesha kusoma pasipo kukaa chini.
Mwita amesema mbunge huyo ni mdau mkubwa wa elimu na mchango wake unaonekana kwa macho namna anavyosaidia kuinua elimu.
" Tunamshukuru sana mheshimiwa mbunge kwa mchango wake wa kutoa madawati kwaajili ya shule zetu za msingi kwa lengo la kufanya kila mtoto kukaa kwenye dawati.
" Huyu sio mbunge wa kuongea sana bali ni mbunge wa kuongea kwa vitendo na sio kwenye elimu pekee bali shughuli mbalimbali za kimaendeleo",amesema",
Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime Malema Sollo aliyekuwepo kwenye tukio la kupokea madawati hayo amempongeza mbunge huyo kwa namna anavyotekeleza ilani kwa vitendo.
Amesema kazi anazozifanya zinaonekana kwa macho na anakitendea haki chama hicho hali ambayo haitawapa kazi ngumu kwenye uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesema licha ya madawati hayo lipo kontena la vifaa vya elimu ya msingi analolileta mbunge huyo kwa shule hizo kama ambavyo alifanya katika sekta ya afya.
Aidha Katibu Mwenezi huyo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa majimbo mawili ya Wilaya ya Tarime kwaajili ya miradi ya maendeleo.
0 Comments