Header Ads Widget

WATOTO NI MIONGONI MWA WATU 18 WALIOUAWA KATIKA SHAMBULIO LA URUSI DHIDI YA MJI WA KRYVYI RIH

 


Shambulio la kombora lililotekelezwa na Urusi katika mji wa Kryvyi Rih ulio katikati mwa Ukraine limeua takriban watu 18 na kujeruhi makumi, maafisa wa Ukraine wamethibitisha.

Tisa kati ya waliofariki ni watoto, alisema Rais Volodymyr Zelensky, ambaye alikulia katika mji huo wa Kryvyi Rih.

Maafisa wa eneo hilo walisema kuwa kombora lilipiga eneo la makazi ya watu.

Picha zilionyesha mtu mmoja akiwa amelala kwenye uwanja wa michezo, huku video ikionyesha eneo kubwa la jengo la ghorofa 10 likiwa limeharibiwa na waathiriwa wakiwa wamelala barabarani.

Wizara ya ulinzi ya Urusi baadaye ilidai "shambulio la kombora lililotekelezwa kwa umahiri wa hali ya juu" lililenga mkutano wa "makamanda wa vitengo na wakufunzi wa mataifa ya Magharibi" katika mkahawa, na kukadiria kuwaua 85.

Hata hivyo haikutoa ushahidi wowote.

Jeshi la Ukraine lilijibu kwa kusema kuwa Urusi inaeneza habari za uongo kwa kujaribu "kuficha uhalifu wake".

Ilisema kuwa Moscow ilirusha kombora la aina ya Iskander-M ili kusababisha madhara na hasara.

Shambulio hilo, mapema Ijumaa jioni, lilikuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi kulenga mji wa Kryvyi Rih tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi mnamo 2022, na linakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump akishinikiza kusitishwa kwa mapigano.

Zelensky aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba takriban majengo matano yameharibiwa katika shambulizi la ijumaa: "Kuna sababu moja tu kwa nini hali hii inaendelea: Urusi haitaki usitishaji wa mapigano, na tunashuhudia."

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI