Na Fadhili Abdallah, Kigoma
WANANCHI wa kijiji cha Kimara kata ya Kinazi wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wamegomea kutumia huduma za maji safi na salama katika mradi uliotekelezwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira (RUWASA) wakipinga bei kubwa inayotozwa kwa wateja wanaopata huduma ya maji kutoka mradi huo.
Wananchi hao wametoa kilio hicho mbele ya Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma,Felix Kavejuru aliyekuwa akifanya mkutano wa hadhara kijijini hapo ambapo wananchi hao wamesema kuwa wameshindwa kulipia gharama kubwa zinazotozwa kupitia mradi huo hivyo wameamua kurudia utaratibu wao wa kuchota maji mtoni.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Kimara, Foibe Edward alisema kuwa kwa sasa wana matatizo makubwa ya upatikanaji wa maji baada ya wananchi wengi kususia mradi uliotekelezwa na RUWASA kutoka na bei ya shilingi 2000 kwa unit kuwa kubwa hivyo wamerudia kutumia maji ya Mto Kazinga, Mto Luiche na mabonde yaliyopo jirani.
Kwa upande wake Jesca Hengahenga alisema kuwa awali walikuwa na mradi wa maji ambao wananchi walitumia juhudi zao kuutekeleza lakini ulikuwa ukikumbwa na changamoto ya miundo mbinu kusombwa na mafuriko ambao wananchi walikuwa wakichota maji bure na kulipa 200 kwa mwezi za kugharamia miundo mbinu lakini baada ya kuja mradi wa RUWASA gharama zimekuwa kubwa na wananchi hawaziwezi.
Akijibu kuhusu malalamiko hayo Mbunge wa jimbo la Buhigwe, Felix Kavejuru alisema kuwa kwa sasa mradi huo unaendeshwa kwa umeme wa TANESCO na ndiyo maana gharama zinafika hivyo kwa UNIT moja na hasa kutokana na idadi ndogo ya wananchi ambao wamekubali kuunganishiwa mabomba na kwamba ameongea na uongozi wa RUWASA Buhigwe kuona namna ya kuweka Mfumo wa umeme jua katika mtambo wa kuzalisha maji ili kupunguza gharama kwa wananchi.
Naye Meneja wa RUWASA wilaya Buhigwe,Mhandisi Golden Katoto alisema kuwa kwa sasa kijiji hicho kinapata huduma za maji kufuatia mradi uliotekelezwa na RUWASA kwa Zaidi ya shilingi milioni 400 ambao unaendeshwa kwa umeme wa TANESCO hivyo mpango uliowekwa ni wananchi kuvuta maji kwenye majumba yao.
Hata hivyo alisema kuwa wananchi wamegoma kulipa kiasi kilichowekwa kwa Uniti moja wakisema ni kikubwa wakiwa na mazoea ya mradi wa awali ambao walikuwa wakilipa shilingi 200 kwa mwezi, ambapo sasa wameshaomba bajeti ili kurekebisha mradi huo kwa kuweka mfumo wa umeme jua ambao utapunguza gharama hizo kwa wananchi.
Mwisho.
0 Comments