Na Hamida Ramadhani Matukio Daima App Dodoma
WAKUU wa Vyuo vya Mafunzo na Ufundi Stadi kutoka Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Tanga pamoja na visiwa vya Zanzibar na Pemba, wamekutana jijini Dodoma kwa mafunzo maalum ya siku tano yenye lengo la kuboresha na kuimarisha mfumo wa ufundishaji wa elimu ya amali na umahili, sambamba na mahitaji halisi ya soko la ajira la sasa.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, ambayo inasisitiza elimu na ujuzi kama msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, amesema lengo kuu ni kuwajengea uwezo wakuu wa taasisi za mafunzo ili wawe na uelewa wa kina kuhusu namna ya kuendesha vyuo kwa ubunifu, uwazi na ufanisi unaolenga kutoa elimu stahiki na yenye tija.
"Mafunzo haya yanawawezesha viongozi kubadili mtazamo wao wa ufundishaji na kuanza kufundisha kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya vijana ambapo unahitaji vijana wanaohitimu wakiwa na ujuzi wa moja kwa moja unaohitajika kwenye soko la ajira," amesema Dkt, Salukele.
Ameongeza kuwa serikali imepokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau wa sekta binafsi wakiwemo wamiliki wa viwanda na taasisi za biashara, wakisisitiza haja ya vyuo kutoa mafunzo yanayoandaa wahitimu kuwa na tija, umahiri na uwezo wa kujiajiri au kuajirika mara moja.
Mafunzo hayo yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (Enabel), kufuatia juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kufungua fursa za ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya elimu na mafunzo.
Kwa upande wake, mshauri mtaalamu kutoka Enabel, Thomas Aikaruwa, amesema mradi huo umelenga kusaidia serikali kuboresha vyuo vya ufundi kwa kuvifanya kuwa vya kisasa na vinavyotoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Enabel inashirikiana kwa karibu na serikali kuhakikisha kwamba walimu wanapatiwa mafunzo ya kisasa, miundombinu inaboreshwa, na wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia,” Alisema Aikaruwa
Na kufafanua "Kuwa shirika hilo litahudumu hadi mwaka 2027 kwenye utekelezaji wa miradi ya mafunzo ya ujuzi.
Naye Mratibu wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Pemba, Othman Zaid Othman, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mafunzo hayo yanawafikia watendaji wote wa elimu katika ngazi ya chini, ili kuongeza ufanisi katika taasisi zao na kutafsiri sera ya elimu kwa vitendo.
“Tunarudi nyumbani tukiwa na majukumu ya kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa watumishi wenzetu. Elimu ya amali ni mwarobaini wa ajira – tusisitize vijana kujifunza ili wajiajiri,” amesema.
Aidha, Dkt. Mahija Waziri kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) amebainisha kuwa Baraza hilo linahakikisha kuwa vyuo vya ufundi vinakuwa na viwango bora vya utoaji wa mafunzo ya ujuzi unaotekelezeka kwa vitendo, kwa kuzingatia sera mpya ya elimu.
Kwa ujumla, kikao hiki kinaashiria hatua muhimu katika mageuzi ya elimu nchini, kikilenga kujenga mfumo imara wa elimu ya amali utakaowezesha vijana wa Kitanzania kuwa wabunifu, wenye maarifa ya vitendo na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
Mwisho
0 Comments