Header Ads Widget

UINGEREZA YATANGAZA MSAADA ZAIDI WA KIJESHI KWA UKRAINE

 

Askari wa Ukraine wakati wa mafunzo mnamo Februari 2025

Serikali ya Uingereza imetangaza itaipatia Ukraine msaada zaidi wa kijeshi wa kima cha dola milioni mia nne na hamsini ambazo zitatumika kununua ndege mpya zisizoendeshwa na marubani na kukarabati vifaru vya kijeshi.

Hayo yalitangazwa katika mkutano ulioendeshwa na Uingereza na Ujerumani wa mawaziri wa ulinzi waliokutana mjini Brussels kujadili namna za kuendelea kuisaidia Ukraine.

Marekani ilikuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Ukraine katika vita na Urusi lakini tangu Rais Donald Trump kuingia madarakani,hilo limebadilika kwa kiasi kikubwa.

Healey alisisitiza kuwa kazi ya kikundi hicho cha Ulaya ni ya msingi katika kuhakikisha Ukraine inawekwa katika nafasi thabiti zaidi ya kujilinda.

“Hatupaswi kuhatarisha amani kwa kuipuuza vita. Ndiyo maana kifurushi hiki kikubwa kilichotangazwa leo kinalenga kuongeza msaada kwa Ukraine katika mapambano yake dhidi ya Urusi,” alisema.

“Mwaka 2025 ni mwaka wa maamuzi kwa Ukraine. Jukumu letu kama mawaziri wa ulinzi ni kuhakikisha wapiganaji wa Ukraine wanapatiwa kila wanachohitaji kwa ajili ya ushindi wao.”

Mfuko huu mpya wa msaada unakuja kufuatia ahadi mbalimbali za kijeshi kutoka Uingereza kwa Ukraine.

Mwezi uliopita, Waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer alitangaza makubaliano ya pauni bilioni 1.6 kwa ajili ya makombora, kufuatia mkutano wa viongozi wa Ulaya uliofanyika London.

Hata hivyo, Chama cha Liberal Democrats kimekosoa kiwango cha msaada huo, kikikitaja kuwa ni “kiasi kidogo” ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Ukraine.

Kimeitaka serikali ya Uingereza kuchukua hatua zaidi kwa kukamata mali za Warusi walioko Uingereza ili kuiongezea Ukraine fedha za msaada.

“Japokuwa tunapongeza msaada wowote kwa Ukraine, kiasi kilichotangazwa leo ni kidogo mno kuweza kukabiliana na ukatili wa vita vya Putin,” alisema msemaji wa masuala ya ulinzi wa chama hicho, Helen Maguire.

Mkutano wa Ijumaa wa Kikundi cha Mawasiliano ya Ulinzi kwa Ukraine unaongozwa kwa pamoja na Healey na waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius.

Hapo awali, mikutano hii ilikuwa ikiandaliwa na waziri wa ulinzi wa Marekani hadi Januari, Donald Trump alipoingia madarakani.

Tangu wakati huo, ikiwa ni ishara ya Marekani kujiondoa kidogo katika masuala ya usalama barani Ulaya, Healey amechukua jukumu la kuwa mwenyekiti wa mikutano hiyo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI