Header Ads Widget

TNC WAANZA MPANGO KULIOKOA ENEO OEVU MALAGARASI

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

SHIRIKA lisilo la kiserikali la  The Nature Conservancy (TNC)  kupitia Program ya TUUNGANE limeanza kutekeleza mpango wa kuokoa eneo la ardhi Oevu ya Malagarasi ambayo imekumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotishia kutoweka kwa wanyama na ndege adimu waliopo eneo hilo.

 Mkurugenzi wa Program ya TUUNGANE, Lukindo Hiza akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa wataalam wa masuala ya kilimo, maji na maliasili kutoka mikoa yaa Kigoma,Tabora na Katavi kwa ajili ya kujadili mpango wa kilimo endelevu chenye tija kinachojali uhifadhi mazingira (RAMI) uliofanyika mkoani Kigoma.

Hiza alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira katika bonde la ardhi oevu la Malagarasi kutokana na kuongezeka maradufu kwa shughuli za kibinadamu hasa kilimo na ufugaji ambapo uharibifu huo unatishia kutoweka kwa ndege aina ya Shoebill (Bungunus) na Statunga.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika mpango huo wanatarajia kutoa elimu ya kilimo chenye tija kwa wananchi wanaoishi kuzunguka eneo hilo, elimu ya uhifadhi na utunzaji mazingira ili kuokoa ekolojia ya eneo hilo na mapitio ya wanyama na kwamba kuachwa kwa eneo hilo bila hatua za dharula za kuliokoa litateketea.

Akizungumzia kutekelezwa kwa mpango huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Uvinza mkoani Kigoma, Masumbuko Kechegwa alisema kuwa halmashauri imekuwa ikitekeleza mpango wa kilimo bora na uhifadhi wa mazingira sambamba na uwepo wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.


Hata hivyo Kechegwa alisema kuwa  bajeti isiyotosheleza imekuwa changamoto kubwa ya Halmashauri kushindwa kutekeleza mipango hiyo katika maeneo yote ya Halmaashauri hivyo kuwepo kwa wadau kunasaidia kufika maeneo mengi ambapo wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kushiriki kulitunza na kulilinda eneo hilo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI