Header Ads Widget

TARURA YATENGEWA TRILIONI 1.192 UJENZI BARABARA MWAKA WA FEDHA 2025/2026

         Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetengewa Sh.Trilioni 1.192 katika mwaka wa fedha wa 2025/2026 kwa ajili ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya barabara nchini. 

Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahim Kibasa,alisema hayo jana kwenye maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Mahali pa Kazi Duniani yanayofanyika kitaifa mkoani Singida kwenye viwanja vya Mandewa ambayo yameandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA).

Alisema fedha hizo zimepangwa kujenga barabara za kiwango cha lami kilometa 893.16 na za changarawe kilometa 12,000 nchi nzima na kwamba bajeti hiyo ni ongezeko kubwa ukilinganisha na Sh.bilioni 246 ambazo TARURA ilitengewa mwaka wa fedha wa 2020/2021.

Kibasa alisema fedha hizo zinatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kama vile Mfuko wa Barabara, tozo za mafuta ya petroli na diseli,miradi ya uboreshaji wa miji (TACTIC), Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu Dar es Salaam (DMDP).

"Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba barabara ambazo zipo katika kila halmashauri zetu zinafunguliwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji katika maeneo ya wananchi," alisema.

Kibasa alisema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 TARURA ilipangiwa kutumia Sh.bilioni 886.3 ambazo zimefanikiwa kujenga barabara za kilometa 278.32 za kiwango cha lami na kilometa 9334 za kiwango cha changarawe.

Aliongeza kuwa TARURA imekuwa ikitumia teknolojia ya ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe ambapo yapo madaraja 401 nchini na kwa Mkoa wa Singida yapo madaraja 34 yaliyojengwa kwa mawe na mkoa wa Kigoma unashika nafasi ya kwanza kwa kujenga madaraja mengi ya mawe ikifuatiwa na Arusha.

"Ujenzi wa madaraja jwa teknolojia ya mawe tunautumia sana kwasababu gharama zinapungua kwa asilimia 60 ukilinganisha na teknolojia nyingine za kutumia kokoto kama ilivyokawaida," alisema.

Kibasa alisema kushuka kwa gharama za ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe kunatokana na kwamba mawe hayo yanapatikana kwenye mazingira ya wananchi ambapo nao wananufaika kwa kipato na hivyo kuinua uchumi wao.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI