Header Ads Widget

RC MTAMBI APOKEA MSAADA WA MAAFA KUTOKA MGODI WA BARRICK NORTH MARA NA WAZABUNI WAKE

Na Shomari Binda-Matukio Daima

MGODI wa dhahabu wa Barrick North Mara na wazabuni wake leo aprili 17,2025 wamekabidhi misaada kwa Mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kwaajili ya wananchi waliofikwa na majanga ya mvua Musoma hivi karibuni.

Wananchi hao zaidi ya Kaya 300 wa Kata 10 za manispaa ya Musoma walifikwa na majanga hayo baada ya kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

 Kanali Mtambi ameahidi kuwa mkoa utasimamia misaada hiyo iweze kuwafikia walengwa waliokusudiwa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ameushukuru mgodi kwa kutoa shilingi milioni 45, 240,000, mifuko 200 ya saruji na magodoro 20 na kuwahakikishia kuwa msaada huo utatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa.   

“Msaada huu umefika wakati muafaka ambapo tunaendelea kurejesha hali ya wananchi walioathirika katika maafa hayo kuwa nzuri zaidi kuliko hali waliokuwa nayo awali kabla ya maafa hayo”

  " Kwa sasa baadhi ya wahanga wa maafa hayo wamesaidiwa kuanza kuishi maisha yao ya kawaida katika maeneo waliyotoka na wale waliokuwa wapangaji wamesaidiwa kwa kulipiwa kodi ya miezi sita kulingana na kodi zao za awali",amesema.

Amesema Baada ya msaada uliotolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan waathirika wengi wamerejea katika hali zao za awali na familia tatu ambazo nyumba zao ziliathirika zaidi zimejengewa nyumba mpya na kupatiwa majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia.

Mtambi amesema bado kuna watu wanaohitaji msaada ikiwemo ukarabati mkubwa wa nyumba zao ili waweze kurejea katika hali yao ya awali na ikiwezekana wapate hali bora zaidi. 

Ametumia fursa hiyo kuzipongeza Kamati ya Usalama na Kamati ya Maafa Mkoa na Wilaya ya Musoma kwa kazi nzuri walizofanya katika utekelezaji wa zoezi la kuwahudumia wahanga wa maafa hayo na kufanikisha kurejesha hali zao za awali kwa wakati. 

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amesema katika maafa hayo jumla ya kata 10 ziliathirika na kaya 319 zenye watu 1,227 ziliathirika na maafa hayo ikiwa ni pamoja na majengo ya taasisi za Serikali, biashara na dini.  


Chikoka ameushukuru Mgodi wa North Mara kwa kusaidia jitihada za Serikali za kuwarejesha wahanga wa maafa hayo katika hali nzuri ili waendelee kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Kwa upande wake Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu North Mara  Francis Uhadi amesema Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na wazabuni mbalimbali waliopo mgodini hapo umetoa msaada wa fedha taslimu na vifaa. 

Uhadi amesema Mgodi unatoa msaada wa fedha tasilimu shilingi 45,240,000,tani kumi za saruji na magodoro 20 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maafa hayo na wanatoa pole nyingi kwa wote waliofikwa na maafa hayo pamoja na viongozi na watumishi wa Serikali ambao walishiriki kwa namna moja au nyingine kutoa msaada wa kibinadamu kwa waathirika hao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI