Header Ads Widget

RAIS WA KENYA WILLIAM RUTO ASHUTUMIWA KWA KUCHOCHEA VITA DRC NA SUDAN

 



Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amezitaka jamii za kimataifa kuwekea vikwazo Rais wa Kenya William Ruto kwa tuhuma za kuchochea mizozo nchini Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kulinda maslahi yake ya kibiashara.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha KTN usiku wa kuamkia leo, Gachagua alidai kuwa Rais Ruto anashirikiana na wanamgambo wa RSF wa Sudan, Mohammed Hamdan Dagalo (Hemedti), pamoja na viongozi wa kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, kwa lengo la kulinda mtandao wa biashara ya dhahabu.

“Nataka kuomba jamii ya kimataifa wazingatie hali hii nchini kwetu. Hatutapata amani wala usalama katika eneo hili endapo hatutamdhibiti Rais William Ruto, ambaye amejaa ubinafsi na tamaa ya kujinufaisha kibiashara katika kanda hii,” alisema Gachagua.

Aliongeza, “Kwa vifo vinavyotokea Sudan, kamanda halisi wa RSF si Hemedti, bali ni William Ruto, kwa sababu ili harakati yoyote ifanikiwe, inahitaji rasilimali. Pesa za dhahabu zinazotokana na Kenya zinatumika kununua silaha na kuua wanawake na watoto.”

Kauli hii ilitolewa siku moja baada ya serikali ya Sudan inayoongozwa na jeshi kupinga mkutano ulipangwa kufanyika London, ikikosoa kutoshirikishwa kwake na mwaliko wa Kenya, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Chad, nchi ambazo Sudan inazishutumu kwa kushiriki katika mzozo huo.

Mnamo mwezi Februari, Sudan iliishutumu Kenya kwa kuwawezesha makundi yanayohusiana na RSF kusaini mkataba wa kisiasa kwa ajili ya kuanzisha serikali mbadala.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI