Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
TAKWIMU za hapa nchini zinaonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kimepungua kwa takribani asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Waziri wa Afya Jenista Mhagama ameyasema hayo leo April 25 , 2025 jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika siku ya Malaria duniani
Amesema Takwimu hizo zinaonesha Mkoa wa Tabora unaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa asilimia 23, ukifuatiwa na Mkoa wa Mtwara wenye kiwango cha maambukizi asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara wenye asilimia 15.
Aidha, amesema mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya malaria kwa chini ya asilimia moja ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar Es Salaam, Iringa, na Singida
Amesema Kuongezeka kwa Mikoa yenye kiwango cha maambukizi ya malaria chini ya asilimia moja, kutoka mikoa 5 mwaka 2020 hadi kufikia mikoa 6 kwa mwaka 2024 na kutoka Halmashauri 36 mwaka kwa 2020 hadi kufikia Halmashauri 51 kwa mwaka 2024.
"Mikoa hii ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Iringa, Dar es Salaam na Mwanza.
Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za kupima ugonjwa wa malaria kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu kwa haraka (mRDT) na dawa za kutibu malaria kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za Afya," Amesema.
Amesema Kuimarika kwa upatikanaji wa dawa na bidhaa muhimu za malaria kwenye vituo vyote vya umma vya kutolea huduma ambapo upatikanaji wa bidhaa hizo ni zaidi ya asilimia 90.
"Ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kuongeza kasi ya kushusha kiwango cha maambukizi ya Malaria nchini, Wizara yangu inaratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Malaria wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2025," Amesema
Na kuongeza "Mpango Mkakati huu umeainisha mikakati sita ya udhibiti wa Malaria, miongoni mwayo ikiwemo mikakati mikuu miwili ambayo ni; Kuzuia maambukizi ya Malaria kwa kudhibiti mbu waenezao malaria kupitia afua mbalimbali na Kuzuia vifo vitokanavyo na Malaria kwa kuhakikisha mgonjwa mwenye dalili za Malaria anapimwa na anayethibitika kuwa na vimelea vya Malaria anapatiwa matibabu sahihi kwa wakati," Amesema .
Msisitizo mkubwa kwa sasa unawekwa kwenye uwekezaji katika udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia jumuishi ikiwemo kutoa kipaumbele katika afua ya usimamizi na udhibiti wa mazingira ili kuzuia mbu kuzaliana kwa kusimamia usafi wa mazingira na unyunyiziaji wa viuadudu vya Kibaiolojia kwenye mazalia ya mbu.
"Napenda nichukue nafasi hii kuishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kutenga fedha, jumla ya Shilingi za Kitanzania bilioni 10 kwa ajili ya kununua viuadudu vya kibaiolojia kutoka kwenye Kiwanda cha viuadudu cha “Tanzania Biotech Products Ltd” kilichopo Kibaha Mkoani Pwani ili kuwezesha utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji viuadudu kwenye Halmashauri zote 184 nchini," Amesema.
"Afua hii ikisimamiwa na kutekelezwa ipasavyo kupitia usimamizi wa Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, itawezesha kudhibiti mbu waenezao magonjwa mbalimbali wakiwemo waenezao malaria, " Amesema
Aidha Anetoa rai kwa watendaji ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kwa dhati Sheria hizo ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni na miongozo iliyopo ili tuweze kudhibiti ugonjwa huu hatari.
Kwa upande wa bidhaa za uchunguzi na tiba ya malaria, Wizara kupitia Bohari Kuu ya Dawa - MSD imeendelea kuhakikisha vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za Afya hapa nchini vinapata dawa za malaria na vitendanishi vya kutosha na kwa wakati ambazo hutolewa bila malipo kwa wananchi.
Mwisho
0 Comments