Wanawake wa Ruaha Mbuyuni wakiwa wamembeba mbunge wa Viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati Katikati .
Na Zuhura Zukhery, Matukio Daima – Iringa.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Iringa, Ritta Kabati, amewapongeza wanawake wa Kata ya Ruaha Mbuyuni, Wilaya ya Kilolo, kwa kuadhimisha Sikukuu ya Muungano kwa kuandaa kongamano la kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, sambamba na kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika kongamano hilo lililobeba jina la White Party Gala, Dkt. Kabati aliwataka wanawake kujenga utamaduni wa kushirikiana na kusaidiana, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwa kumuunga mkono mwanamke yeyote atakayejitokeza kuchukua fomu za kugombea uongozi.
Alieleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili wanawake ni kutopendana, hasa mmoja wao anapopata mafanikio, hali inayowapelekea wengine kuwa maadui na kuwakatisha tamaa wanawake wenzao katika kufikia ndoto zao.
"Ni muhimu wanawake tukapendana na kushirikiana katika maendeleo. Ukiona mwanamke mwenzio ana ndoto ya kufikia malengo fulani, basi muunge mkono badala ya kumpiga vita. Tuache tabia za kichawi za kuangushana," alisema Dkt. Kabati.
Aidha, aliwahimiza wanawake kuiga mfano wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameonyesha upendo mkubwa kwa wanawake, hususan kwa kuwapa nafasi za uongozi katika serikali yake.
Katika hatua nyingine, Mbunge Kabati alichangia shilingi 500,000 kwa ajili ya kutunisha mfuko wa kikoba kilichoanzishwa na wanawake hao wa Ruaha Mbuyuni, huku naye akijiunga rasmi kuwa mwanachama wa kikoba hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa maandalizi ya sherehe hizo, Mwende Luvinga, alisema wameandaa kongamano hilo kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Muungano, likilenga kuwahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, pamoja na kuwahimiza kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila uoga.
Luvinga alieleza kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake, kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata katika nafasi ya juu ya uongozi nchini.
Akigusia suala la ukatili dhidi ya watoto, Luvinga alisema migogoro ya kifamilia imechangia ongezeko la watoto wa mitaani, huku akiwataka wazazi kutojihusisha na tabia ya kuhamishia migogoro yao kwa watoto, kwa kuwa hali hiyo huwapa watoto msongo wa mawazo na mara nyingine kuwasukuma kuishi mitaani.
"Hakuna mtaa unaozalisha watoto wa mitaani. Ukatili unaotokea majumbani mwetu ndiyo unaosababisha watoto wengi kukimbilia mitaani na hatimaye kukumbana na ukatili mkubwa zaidi," alisema.
Naye mkazi wa Ruaha Mbuyuni, Alisi Thomas, alisema kuwa kongamano hilo limekuwa msaada mkubwa kwa wanawake katika kujitambua, kujitegemea, na kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Katika kongamano hilo, wadau mbalimbali walitoa mada za kuwajengea wanawake uwezo wa kushinda changamoto za kisaikolojia, huku wakihamasisha wanawake hao kuachilia maumivu ya moyo na kufungua ukurasa mpya wa maisha yao.
0 Comments