Header Ads Widget

MAHAKAMA YA MAREKANI YAAGIZA KUREJESHWA KWA MHAMIAJI ALIYEPELEKWA EL SALVADOR KIMAKOSA

 


Mahakama ya juu ya Marekani imeamuru utawala wa Rais Trump usimamie kurejeshwa kwa mhamiaji aliyepelekwa El Salvador mwezi uliopita baada ya kutuhumiwa kimakosa kuwa mwanachama wa genge la wahalifu wa kutoka Amerika Kusini.

Familia ya Kilmar Abrego Garcia ilipinga mahakamani uhalali wa kurejeshwa kwake El Savador,akiwa sehemu ya kundi la wahamiaji zaidi ya mia mbili wanaoshutumiwa kuwa na mafungamano na magenge ya wahalifu waliotupwa gerezani El Salvador na wanatarajiwa kukaa huko kwa mwaka mmoja.

Kesi hiyo sasa inarejeshwa katika mahakama ya mwanzo, huku majaji wa ngazi za juu wakikosa kuweka kikomo cha muda kwa serikali kuhusu lini Garcia anapaswa kurejeshwa nchini.

Garcia, mwenye umri wa miaka 29, aliingia Marekani kinyume cha sheria akiwa kijana kutoka El Salvador.

Mnamo mwaka 2019, alikamatwa pamoja na wanaume wengine watatu huko Maryland na kuwekwa kizuizini na maafisa wa uhamiaji wa shirikisho.

Ingawa kulikuwa na sababu za kisheria za kumrejesha nchini kwao, jaji wa uhamiaji alimpa hifadhi dhidi ya kufukuzwa, akizingatia uwezekano wa kuteswa na magenge hatari ya mitaani katika nchi yake ya asili.

Hata hivyo, licha ya amri ya mahakama iliyopiga marufuku kuondolewa kwake, Garcia alifukuzwa nchini Marekani tarehe 15 Machi.

Mkewe, Jennifer Vasquez Sura ambaye ni raia wa Marekani amekuwa mstari wa mbele kupaza sauti akiitaka serikali kumrejesha mumewe.

“Hali hii imekuwa kama safari ya kihisia isiyotabirika kwa watoto wangu, mama ya Kilmar, kaka yake pamoja na ndugu zake wote,” Bi. Sura aliambia gazeti la New York Times siku ya Alhamisi.

“Nitaendelea kupigana hadi pale mume wangu atakaporejea salama nyumbani,” aliongeza kwa msisitizo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI