Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati wananchi wakilia na changamoto ya ubovu wa Miundombinu ya barabara hususani katika kipindi hiki cha masika Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani Njombe wameutaka Wakala wa barabara mijini na vijijini Tarura kuchukua hatua za haraka kushughulikia maeneo korofi yanayokatisha mawasiliano.
Katika Kikao Baraza la madiwani Cha robo ya Tatu ya Mwaka wa Fedha wa 2025/2026 madiwani hao akiwemo Paulo Kinyamagoha, Innocent Gwivaha na Neema Mbanga wamesema hali ya barabara kwa sasa ni mbaya na wakati mwingine Tarura wanapochelewa kufika mawasiliano yanakatikana na kukwamisha Uchumi wa wananchi na Serikali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli Ametaka kufanyiwa kazi kwa barabara ambazo zinakwama ili ziweze kupitika licha ya mvua kuendelea.
Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo Meneja wa Tarura wilaya ya Njombe Mhandisi Costantine Ibengwe amesema wameendelea kuchukua hatua za haraka kufungua barabara zinazokatisha mawasiliano pindi wanapo pata taarifa huku wakisubiri mvua ziishe ili waendelee na marekebisho makubwa.
Naye Mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda mbali na changamoto ya barabara lakini amewasisitiza suala la usimamizi wa miradi ya Maendeleo yakiwemo maboma kukamilishwa yote yaliyopata Fedha.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe George Makacha amesema wataendelea kuongeza jitihada katika makusanyo ya ndani ili wafikie malengo waliyojiwekea.
0 Comments