Na Lilian Kasenene,Morogoro
Matukio DaimaApp
KATIKA kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025,Waandishi wa Habari nchini wamehimizwa kuzingatia maadili na weledi katika utendaji wao wa kazi wakati wa kuripoti habari za uchaguzi Mkuu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.
Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari nchini (JOWUTA) Mussa Juma alitoa wito huo wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha pamoja mkoani Morogoro Waandishi wa Habari kutoka Mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro.
Mwenyekiti huyo wa Jowuta aliwataka Waandishi wa Habari pia kuacha kuegemea chama chochote cha siasa pamoja na kuhakikisha wanajilinda dhidi matukio yenye kuhatarisha usalama wao na vifaa vyao vya kazi.
Alisema mafunzo hayo ni mahususi kuwajengea uwezo waandishi kuripoti uchaguzi kwa Amani, kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa, usalama wao wenyewe kabla, wakati na baada ya uchaguzi Mkuu.
“Tunataka waandishi wasiwe na upendeleo katika vyama vya siasa, watoe fursa sawa kwa vyama vyote kipindi chote cha uchaguzi, tumekutana kuwakumbusha pia suala la usalama wao wakati wa uchaguzi ili uchaguzi unapomalizika wabaki salama, jinsi gani wanaweza kujilinda na majanga mbalimbali, tumewaelekeza jinsi ya kujilinda na majanga ya mtandaoni,”alisema Mussa Juma
Aidha Mwenyekiti huyo, alihimiza Viongozi wa Vyama vya Siasa kuheshimu wanahabari katika kipindi chote cha kampeni, ambapo kwa miaka ya nyuma kumekuwa na vitendo vya baadhi ya vyama vya siasa kuwashusha wanahabari kwa tuhuma ya kuandika habari za chama kingine kuelekea uchaguzi Mkuu.
Alisisitiza Wanahabari wapewe uhuru katika kuhabarisha umma wakati wote wa uchaguzi pasipo kubugudhiwa ili kuwa sehemu ya kuwaimarishia ulinzi wao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwandishi wa Habari kutoka Habari Faster, Emiry Mwaipopo alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutosha katika kuhakikisha hawaandika habari zenye kuegemea chama kimoja cha siasa, watazingatia weledi katika utendaji wa majukumu yao pamoja na kuzingatia kalamu ya mwandishi kutokuwa sehemu ya kusababisha, kuchochea wala kuleta machafuko.
“Nimejifunza vitu vingi ikiwa ni pamoja na kutumia kalamu yangu vizuri, kuandika habari ambazo hazileti machafuko, zenye uzalendo na kuepusha chuki kwenye Taifa letu,”alisema Mwaipopo.
Naye Mjumbe wa Bodi Baraza la Waandishi wa Habari Afrika (Congress of African Journalists (CAJ) Idda Mushi alisema wanahabari wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kuandika habari zisizo leta sintofahamu kwa jamii.
Mushi alisisitiza kuwa wakati ni sasa wanahabri kujiweka sawa katika kuhabarisha habari za uchaguzi kwa usahihi kabla, wakati na baada ya uchaguzi Mkuu.
Akifungua mafunzo hayo Afisa Uchaguzi Manispaa ya Morogoro Shabani Duru alitumia mafunzo hayo kwasisitiza Waandishi wa Habari kuwa na mashirikiano ya karibu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC wakati wa kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema Waandishi wa Habari ni miongoni mwa wadau wakubwa wa masuala ya uchaguzi hivyo ni vyema wakatekeleza majukumu yao kwa ukaribu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) kupata msaada wa miongozo, taratibu na kanuni zote za uchaguzi.
Mafunzo hayo kwa Waandishi wa Habari yamedhaminiwa na Shirikisho la Waandishi wa Habari Duniani(International Federation of Journalists(IFJ) pamoja na Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika(FAJ) kwa kishirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Taasisi ya wanahabari ya kusaidizi jamii za pembezoni(Media Aid for Indegenous and Pastoralist Community(MAIPAC).
Waandishi wa Habari kutoka Kanda tatu za mashariki wameanza kupata mafunzo hayo, ikifayiwa na Nyanda za juu kusini pamoja na Kaskazini.
Mwisho.
0 Comments