Uongozi wa Klabu ya ligi kuu Zanzibar, Junguni United FC umetangaza kuwasimamisha na kuwafukuza wachezaji saba kwa makosa ya kushiriki katika upangaji wa matokeo kupitia kubashiri (sports betting), kinyume na sheria na maadili ya mchezo wa soka.
Katika taarifa iliyotiwa saini na Katibu wa klabu hiyo, Suleiman Mwidani, wachezaji waliokumbwa na adhabu hiyo ni: Salum Athumani Chubi, Ramadhani Ally Omar, Abdallah Sebastian Ponera, Danford Moses Kaswa, Bakar Athumani Jomba, Rashid Abdallah Njete na Iddi Said Korongo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wachezaji husika walibainika kuhusika katika ubashiri wa matokeo ya mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar 2024/2025 dhidi ya klabu za Malindi na New City, kinyume na Katiba ya klabu na kanuni za ligi hiyo (kifungu cha 23, kipengele cha 2 na 3).
Uchunguzi wa ndani uliofanywa na uongozi wa klabu ulithibitisha uvunjaji huo wa sheria, na hivyo klabu ikaamua kuchukua hatua kali kwa mujibu wa taratibu zake.
"Baada ya kujiridhisha kuwa wamevunja sheria, tumeamua kuwasimamisha mara moja kucheza mpira wa miguu ndani ya Junguni United FC wala kujihusisha na shughuli yoyote ya klabu," taarifa hiyo ilieleza.
Uongozi wa Junguni United FC pia umetangaza kuwa umeshapeleka taarifa za tukio hilo kwa vyombo vya kisheria na kwa mashirikisho ya soka husika, ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya waliohusika, pamoja na wengine wanaoendeleza tabia hiyo inayodhoofisha maendeleo ya soka Zanzibar.
"Tunaomba mashirikisho ya soka kuchukua hatua za kisheria ili kuikomesha tabia hii inayorudisha nyuma maendeleo ya mpira wetu," amesisitiza Katibu wa klabu.
Hatua hii imepongezwa na wadau mbalimbali wa michezo Zanzibar na nje ya Zanzibar, wakieleza kuwa ni mfano wa kuigwa katika kulinda heshima na uadilifu wa mashindano ya soka visiwani.
Katibu wa klabu ameiambia BBC kwa ufupi kwamba "ilitulazimu tufanye hivyo maana hali imekuwa tete".
0 Comments