NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amefanya ziara ya kikazi jimboni na kugawa miche ya migomba ya kisasa elfu kumi (10,000,000) ijulikanayo kwa jina la FIAH 17 kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Kata.
Viongozi hao walipokea miche hiyo kwa niaba ya wananchi wa Kata wanazotokea ambapo miche hiyo ilitolewa kwa Kata 14 za ukanda wa milimani ambako migomba hulimwa.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa mbegu hizo Mbunge Ndakidemi alisema kuwa Jimbo la Moshi Vijijini ukanda wa Milimani una ardhi na mazingira bora kwa kilimo cha migomba na mbegu aliyowapa itaenda kuongeza uzalishaji ambapo mkungu mmoja unaweza kufikisha kilo 150 hadi 200 ukilinganisha na migomba iliyopo ambayo wanavuna kati ya kilo 10 hadi 50.
"Wakati wa Kampeni niliahidi kuleta migomba hii, na nimewasiliana na taasisi ya kimataifa ya The International Institute of Tropical Agriculture (IITA) ambayo imenipa ufadhili wa mbegu hizi kupitia kwa Profesa Rony Swenen, niliona kuna haja ya kuleta mbegu hizi ili kukuza uzalishaji wa zao hili" alisema Ndakidemi.
Mbunge huyo amewataka Viongozi hao kugawa miche waliyopewa kwa usawa kwani imetolewa kwa ajili ya wananchi.
Akiongea kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Andrew Mwandu alimshukuru Mbunge kwa kutekeleza ahadi yake kwa wapiga kura wake.
Tokea mbunge achaguliwe, ameshagawa miche elfu kumi na sita (16,000) kwa wakulima wa Jimbo la Moshi Vijijini.
Wakishukuru kwa niaba ya viongozi wenzao, Katibu wa CCM Kata ya Mbokomu Sofia Mshiu na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Oldmoshi Mashariki Ronald Tenga walisema mbegu hizo bora za Migomba zitasaidia wakulima kuzalisha kwa tija na kuongeza mapato ya kaya.
Mwisho.
0 Comments