Zaidi ya mwezi mmoja baada ya kufungiwa katika Hoteli ya Decapolis huko Panama City, makumi ya wahamiaji wa Asia na Kiafrika waliofukuzwa kutoka Marekani wanabaki Panama, kwa kukosa mahala pa kwenda.
Ni wanaume, wanawake, na watoto kutoka nchi zikiwemo Iran, Afghanistan, Nepal, Pakistan, Somalia, Eritrea, Cameroon, Ethiopia, China, na Urusi, msemaji wa Fe y AlegrÃa (Imani na Furaha), shirika la kidini ambalo kwa sasa limewapokea 61 kati yao katika Jiji la Panama, aliiambia BBC Mundo.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka kwa serikali ya Panama, wahamiaji 192 kati ya 299 waliowasili Panama baada ya kufukuzwa kutoka Marekani wamekubali kwa hiari kurudi katika nchi zao.
Wahamiaji wengine walipokea kibali cha muda cha kibinadamu cha siku 30, ambacho kinaweza kuongezwa kwa siku nyingine 60. Baada ya kipindi hiki, wanaweza kufukuzwa kutoka Panama.
BBC ilizungumza na wahamiaji watatu nchini Panama, Wairani wawili na raia mmoja wa Afghanistan, ambao walisema walikuwa katika hali mbaya. Hawana pesa na hakuna pa kwenda.
Wote watatu wanakubali kwamba kurudi katika nchi yao sio chaguo.
"Mnamo 2022, niliamua kubadili dini yangu na kuwa Mkristo. Nchini Iran, adhabu ni kifo," Artemis Ghasemzadeh aliambia BBC.
Juanita Goebertus, mkurugenzi wa Amerika katika Human Rights Watch (HRW), aliambia BBC Mundo kwamba shirika hilo limetambua kesi za mtu binafsi " zenye dalili za wazi za mateso, ambayo yanazuia watu hawa kurejeshwa katika nchi zao za asili bila kuweka maisha yao hatarini."
Serikali ya Panama imesema kuwa wahamiaji ambao hawawezi kurejea katika nchi yao ya asili watalazimika kutafuta nchi ya tatu iliyo tayari kuwapokea.
0 Comments