Na Shomari Binda-Musoma
DIWANI wa Kata ya Makoko na Meya wa manispaa ya Musoma Patrick Gumbo ameelezea namna kituo cha afya kilichojengwa kwenye Kata hiyo kilivyosaidia utoaji huduma za afya.
Akizungumza na Matukio Daima leo aprili 3,2025 kuhusiana na huduma za kijamii ndani ya Kata hiyo zinavyotolewa zikiwemo za afya amesema hawana shida juu ya upatikanaji na utoaji huduma hizo baada ya kupata kituo hicho.
Amesema huduma muhimu za mama na mtoto zinazotolewa kwenye kituo hicho kwa ufanisi mkubwa zikiwemo huduma nyingine za kulazwa wagonjwa.
Gumbo amesema wananchi wa Kata ya Makoko na maeneo jirani ya kituo hicho wanapata huduma na kuepuka kwenda kwenye hospitali ya manispaa au hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
" Kituo hiki cha afya kimekuwa msaada kwa wananchi ndani ya Kata na majirani zetu wanao tuzunguka wakiwemo hadi wa Musoma vijijini.
" Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha za ujenzi wa kituo hiki cha afya ambacho sasa kinatoa huduma saa 24",amesema.
Licha ya kuzungumzia huduma za afya Gumbo amesema huduma nyingine za kijamii zimeboreshwa ndani ya Kata ikiwemo miundombinu.
Amesema maji yanapatikana kwa asilimia 98,elimu shule mpya imejengwa na barabara nyingi zimefunguliwa ikiwa ni pamoja na kujengwa vivuko na madaraja inayowezesha wananchi kupita kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Makoko wameshukuru juhudi za diwani wao kupambania shughuli za maendeleo na huduma za afya wanazozipata kwenye kituo cha afya kilichopo ndani ya Kata yao.
Magesa Juma mmoja wa wananchi wa Kata Makoko mkazi wa Mtaa wa Ziwani amesema licha ya huduma za afya wazozipata kwenye kituo cha afya lakini waganga na wauguzi wamekuwa na kaull nzuri na kuwapokea kwa upendo wanapokwenda kupata huduma.
MWISHO
0 Comments