Na Matukio Daima Media
Baraza la wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) mkoa wa Songwe limetoa azimio la kubariki kampeni ya No reforms no election kwa madai kuwa ni kauli mbiu isiyopingika kwani wananchi wanahitaji kuwa na sheria nzuri zihusuzo chaguzi katika kupata viongozi wanaowataka.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Baraza hilo mkoa wa Songwe Agness Atanas Chilulumo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Tunduma mkoani Songwe akisema kwa mtu yeyote mwenye akili timamu lazima aunge mkono kampeni hiyo na kukemea kile alichokiita kuibuka kwa kundi la G55 na kupinga maamuzi ya Chama hicho Taifa ya kutaka kuzuia uchaguzi mkuu.
"Kuna kikundi ambacho kimeibuka ndani ya Chama (CHADEMA) kwa sababu mimi nawezakukiita ni kikundi cha waasi. Sisi hawa hata ukisoma kwenye maandiko tunawafananisha na akina kola ili kuififisha agenda hii. Hiki ni kikundi cha watu wachache hatujui wana ujasiri gani hadi kuibuka na kupinga maamuzi ya kamati kuu ya Chama hivyo chama kinatakiwa kuchukua hatua dhidi yao maana hii ni agenda ya wa-Tanzania", ameeleza Agness Chilulumo, mwenyekiti wa BAWACHA mkoa wa Songwe.
Aidha kiongozi huyo amewataka wananchi kuendelea kuungana na CHADEMA na kutoteteleka kwa namna yoyote badala yake waungane kupigania upatikanaji sheria nzuri za kusimamia chaguzi na kuwa na tume huru ya uchaguzi ili kuwa na chaguzi za huru na haki.
Pia amewaomba kuendelea kukichangia chama hicho ili kujiendesha kupitia kampeni yake ya Tone Tone.
Pamoja na hayo, mwenyekiti wa BAWACHA mkoani Songwe amelitaka jeshi la Polisi nchini kutokukubali kutumika vibaya na Chama tawala (CCM) kwenye masuala ya kisiasa bila kuzingatia sheria akidai Polisi inatumika ili kusaidia Chama hicho.
Aidha amekemea nguvu iliyotumiwa na jeshi la Polisi wakati wa kuwakamata mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Antipas Lissu na baadaye makamu mwenyekiti wa CHADEMA Taifa (Bara) John Heche na wengineo kabla ya kuwachia huru baadaye na kumfikisha mahakamani mwenyekiti Lissu akisema ni kukosa weledi kwa jeshi la Polisi kumkamata kiongozi wa kisiasa kana kwamba ni mwizi au jambazi
Amesema sio sahihi jeshi kuingizwa kwenye masuala ya kisiasa badala ya kusimamia eneo lake kuu la ulinzi wa raia na mali zao akidai wanatumika na Chama Cha Mapinduzi.
Kwa upande wake katibu wa BAWACHA mkoa wa Songwe Pendo Mwashiuya, amesema wanawake wa mkoa wa Songwe wako tayari kuandamana kwa namna yoyote kuhakikisha uchaguzi mkuu haufanyiki kutokana na sheria zisizo rafiki za kiuchaguzi kutokuwa rafiki.
0 Comments