Na Hamida Ramadhan Matukio Daima app Dodoma
KATIKA kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi Januari, 2025, Tume ya madini imejiwekea vipaumbele vyake vikiwemo
Kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini pamoja na kuvutia uwekezaji.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 4 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Kipaumbele kingine nipamoja na Kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa kuendelea kuboresha mazingira yatakayowezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini.
Ameeleza kipaumbele kingine Kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano kati ya Tume na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini;
Kuendeleza rasilimali watu na kuboresha ustawi wa watumishi.
Kuhamasisha uwekezaji ,uanzishwaji wa minada,maonesho ya madini ya vito na uongezaji thamani madini; na
Kuendeleza madini muhimu na madini mkakati.
MAFANIKIO YA TUME YA MADINI
Mafanikio ya Tume ya Madini kwa kipindi cha 2021/2022 hadi Januari, 2025 ni pamoja na:
Amesema nipamoja na kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na rasilimali madini, kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini.
Amesema kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024.
"Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu, " Amesema Mhandisi Lwamo
Aidha katika kipindi cha kuanzia Julai, 2024 hadi Februari, 2025, Tume imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 690,763,401,639.06 sawa na aslimia 69.08 ya lengo la Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Hata hivyo amebainisha Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023.
"Hii ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za Madini ambapo ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023,"
Na kuongeza "Kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Madini, mwenendo wa Mchango wa Sekta ya Madini na ukuaji wake unatarajiwa kufikia asilimia 10 na zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025," Amesema Mhandisi Lwamo
Sambamba ba hilo tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini, wasambaza bidhaa na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123.
"Katika kipindi rejewa, jumla ya Mipango 1,076 ya Ushirikishwaji wa Tanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,047 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 29 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho, " Amesema
Aidha Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa Ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Kampuni mbalimbali za uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,874 ambapo kati ya hizo 19,371 ni Watanzania sawa na asilimia 97.5 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.5 ya ajira zote zilizozalishwa.
Vilevile amesema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.
Katika kuendelea kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini, Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi rejewa, Tume imefanikiwa kutenga maeneo 58 kwa ajili ya Wachimbaji wadogo katika Mikoa mbalimbali.

0 Comments