Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida (SINGPRESS) kimemshukru Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Singida,Chifu Thomas Mgonto kwa futari aliyoiandaa kwa ajili ya waandishi wa habari wa mkoa huu.
Mwenyekiti wa SINGPRESS Mkoa wa Singida, Elisante John, alitoa shukrani hizo jana kufuatia Chifu Mgonto kuamua kuwafuturisha wanahabari hao.
"Tunamshukru sana Chifu Mgonto kwa futari hii ni jambo jema wewe unekuwa mdau wa kwanza kufanya jambo hili tunaomba na wadau wengine waige mfano huu CCM imeonesha mfano kupitia kwako," alisema John.
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwataka watu wanaofanya kazi ya uandishi wa habari lakini hawajasomea taaluma hiyo kujiendeleza kielimu kwani kuzinduliwa na kuanza kufanya kazi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ni wazi kuwa itakuwa vigumu kwao kuendelea kufanya kazi hiyo bila kuwa na elimu.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari ilizinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ikiwa na jukumu la kusimamia viwango vya kitaaluma na maadili vinazingatiwa kwa Waandishi wa Habari.
Elisante alisema ili kuendelea kuiheshimisha tasnia ya uandishi wa habari pamoja na kujenga weledi, nidhamu na maadili kitaaluma na jamii kwa ujumla waandishi wa Habari wanatakiwa kujiendeleza kielimu.
Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa habari kwamba baadhi ya waandishi wa habari wanaandika mambo ambayo hayaeleweki jambo ambalo linafedhehesha taaluma hiyo ambayo ni muhimili wa nne usiokuwa rasmi.
"Hapa bado kuna vijana wadogo sana mwezi Aprili umekaribia si mumeona Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imezinduliwa itakuja kutong'oa tusiokuwa na taaluma ya uandishi tujitahidi kujiendeleza kielimu," alisema.
Alisisitiza kuwa anafahamu wapo baadhi ya waandishi wana vyombo vyeo binafsi walivyoanzisha lakini wajitahidi kutekeleza majukumu yeo kwa ufanisi hapo watakuwa wameujengea heshima Mkoa wa Singida.
Aidha,Mwenyekiti huyo wa SINGPRESS alimpongeza Chifu Mgonto kwa uamuzi wake wa kufuturisha waandishi wa habari na kuwataka wadau wengine kuiga mfano huo .
Naye Katibu wa Chief Mgonto Foundation,Kasimu Mumbawa alisema wameandaa futari hiyo ili kuendeleza mahusiano mema hasa ikizingatia kuwa waandishi wa habari wamekuwa ni chachu ya maendeleo kutokana na kutoa taarifa mbalimbali za serikali na za jamii kwa ujumla.
"Sisi kama Chief Mgonto Foundation tuna kitengo cha kukaa na watu kushauriana na kutoa maoni mbalimbali lakini yote tunayoyafanya hatujawahi kuwaacha waandishi kwasababu tunatambua wao ndio mtaji na nguzo muhimu sana katika maendeleo," alisema.
Naye Chifu Francis Nghe'ni ambaye alimwakilisha Chifu Mgonto alisema waandishi wa habari ndio wajenga nchi hivyo ni watu muhimu na kwamba taasisi ya Chief Mgonto Foundation itaendelea kushirikiana na wana habari.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu 2025 ni matumaini kuwa waandishi wa habari wataweza kutekeleza majukumu yao vyema kwa kutenda haki kwa wagombea wote watakaotia nia.
0 Comments