Header Ads Widget

WANANCHI WATAKA SAMIA LEGAL AID IENDELEE KUTATUA MIGOGORO.

 


Wakazi wa vijiji vya Chokaa na Mapogoro kata ya Chokaa huko Chunya mkoani Mbeya, wameishukuru Serikali kwa kutuma wataalam wa sheria kwenda kusikiliza kero zao kuhusu masuala ya ardhi na ndoa kutokana na kukithiri kwa migogoro katika jamii na kuomba kampeni hiyo iwe endelevu ili kuongeza kasi ya kutatua migogoro inayoikabili jamii.

Wakizungumza katika kitongoji cha Sambilimwaya kijiji cha Chokaa wilayani Chunya, wananchi katika kitongoji hicho wamesema wamekuwa wakikabiliwa na migogoro mingi ya ardhi na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili katika ndoa lakini wamekuwa wakikosa msaada na kujikuta wakiangukia hatua mbaya ikiwemo mauaji inayochochewa na migogoro ya ardhi.

Wamesema elimu hiyo ya kisheria kupitia wizara ya Katiba na sheria imekuja kwa wakati muafaka ili kuwasaidia kutatua migogoro inayowakabili hususani waliouziwa maeneo yao bila ushirikishwaji yakidaiwa kuwa ni maeneo ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu hasa wa zaidi ya miaka 12.






"Mfano mimi nina ekari zaidi ya arobaini lakini Serikali ya kijiji wamekuja kuuza maeneo yangu ya pembeni mimi nimebaki katikati, nilisema niwaachie eneo fulani pale kwenye eneo langu lakini bado wanauza na kwingine mimi naomba tu wanirudishie maeneo yangu maana wakisema sijaendeleza ni kweli silimi yote lakini nimesafisha halafu nina watoto nane na wajukuu hivyo nitajitahidi kuwagawia watoto wajenge", ameeleza bi. Grace Kawelu mkazi wa wilayani Chunya..

Mwenyekiti wa kijiji cha Chokaa Ernest Mwakibete, amesema Serikali ilielekeza mapori ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu yagawiwe kwa wananchi ambao hawana maeneo ya kufanyia shughuli zao hasa za kilimo na wanaohitaji kununua hivyo Serikali ya kijiji imekuwa ikiwahusisha wananchi wenye ardhi husika kwa wenye maeneo kama wapo waliyokuwa wakimiliki na kuafikiana ili kubaki na maeneo ambayo wana uwezo wa kuyaendeleza na kuwa mapori ya wazi ndio yamekuwa yakilengwa hasa.

Mwenyekiti Mwakibete, amesema kwa ngazi yake ya kijiji ameendelea kushirikiana na wenzake kutatua kero mbalimbali za ardhi, kero ambazo zimeibuka kwa kipindi cha hivi karibuni hasa kutokana na himizo kubwa kwenye sekta ya kilimo.

Kwa upande wake mwanasheria/wakili katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya Jackline Massawe, amewataka wananchi wanapokuwa na tofauti zozote basi wafuate taratibu kuzitafutia ufumbuzi ili kuepusha migogoro mikubwa na ugomvi ambao umekuwa ukiibuka maeneo katika mengi kutokana na masuala ya ardhi na ndoa kwa sehemu kubwa.

Moli Masoud ni afisa ardhi wilaya ya Chunya, amesema ujio wa kampeni ya mama Samia Legal Aid ni kuhakikisha inatatua migogoro hiyo ambayo imekuwa ikitatuliwa pia na Serikali ambapo katika wilaya yake amehimiza wananchi kumiliki maeneo yao kisheria na kukubali kuwa na maeneo ambayo wana uwezo nayo na kutovamia maeneo yasiyo ya kwao ili kuepusha migogoro inayoepukika.

Elimu mbalimbali zimetolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji cha Sambilimwaya kijiji cha Chokaa na baadaye kufanyika katika kijiji cha Mapogoro ambapo pia elimu hiyo imetolewa ikiwemo masuala ya ukatili na unyanyasaji kwenye ndoa na kwa watoto na kuhakikisha watoto wanasomeshwa kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.

Timu ya mama Samia Legal Aid inalenga kutoa elimu na ushauri wa masuala mbalimbali yahusuyo sheria, ndoa na mirathi ikiwemo pia kuwasikiliza mwananchi mmoja mmoja ambapo tangu kuanza kwa kampeni hiyo ya kitaifa watu mbalimbali wamesaidika kwa kutatuliwa na kushauriwa kero zilizokuwa zikiwasibu.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI