Header Ads Widget

TCCIA: WAJASILIAMALI WENGI HAWAJUI TARATIBU BIASHARA ZA KUVUKA MPAKA

Mratibu wa shirika la Mapinduzi ya kijani Afrika (AGRA)  Donald Mizambwa

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

ZAIDI ya asilimia 70 ya wafanyabiashara vijana na wanawake  wanaofanya biashara ya kuvuka mpaka kwenda nchi za Afrika Mashariki na nchi za Maziwa Makuu hawajui taratibu zisizo za kikodi za kushughulikia vibali kwa ajili ya kufanya biashara hizo jambo lililofanya wafanyabiashara wengi kukwama na biashara zao kutokuwa na mafanikio.

Meneja ufuatiliaji na tathmini kutoka Chama Cha Wafanyabiashara, wenye viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa Kigoma,Dk.Chaboba Mkangwa alisema hayo katika mkutano wa majadiliano kupitia mradi ujasiriamali wa vijana kwa mustakabali wa chakula na kilimo (YEEFA) kuhusu changamoto zisizo za kikodi za biashara za kuvuka mpaka (NTBs)  zinazowapa wafanyabiashara wadogo na wa kati vijana na wanawake.

Dk.Mkangwa alisema kuwa wafanyabiashara wengi vijana na wanawake wameingia kwenye biashara bila kuwa na utafiti wa kutosha wa biashara wanayokwenda kufanya katika nchi nyingine, hawajui taratibu za kushughulikia vibali vya biashara zao na hivyo wengi kukwama na kukata tamaa ya kufanya biashara za kuvuka.

Mtaalam huyo wa masuala ya biashara alisema kuwa pamoja na hilo pia matumizi ya mabavu na urasimu unaofanywa na watendaji wa mamlaka za serikali kwenye maeneo ya forodha imekuwakikwazo kikubwa cha biashara ya kuvuka huku vijana na wanawake wenye mitaji midogo wakiwa wahanga wa changamoto hizo.

Akizungumza katika mkutano huo wa majadiliano Mratibu wa shirika la Mapinduzi ya kijani Afrika (AGRA) ambao ndiyo wanaofadhili utekelezaji wa mradi huo, Donald Mizambwa alisema kuwa mradi umekuja ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kuweza kuongeza chachu kwa vijana na wasichana kufanya biashara ya kuvuka mpaka.


Mizambwa alisema kuwa katika changamoto hizo pia wataangalia namna ya kuwapa maelekezo ya wapi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao wanapopata vikwazo, taratibu za kufuata kuweza kukamilika taratibu za biashara za kuvuka mpakan lakini pia kuwaunganisha wafanyabiashara hao na taasisi za fedha kuona namna ya kupata mikopo ambayo itainua biashara zao hasa zinazohusu mazao ya kilimo kwa ajili ya uhakika wa chakula.

Akifungua mkutano huo Katibu Tawala Msaidizi huduma za biashara na uchumi mkoa Kigoma, Deogratius Sangu akimwakilisha Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Ruga alisema kuwa vijana na wanawake wana nafasi kubwa ya kufanya biashara na nchi nyingine kwa mafanikio na kwamba ipo kila sababu ya kushughulikiwa kwa vikwazo hivyo ili biashara zao ziwe na tija.


 Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI