NA HAMIDA RAMADHAN MATUKIO DAIMA APP DODOMA
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto 54 na kufanya idadi ya walionufaika kufikia 88 tangu kuanzishwa huduma hiyo nchini Juni 2017.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Rachel Mhaville ameyasema hayo Leo Machi 6 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Amesema Serikali imewagharamia watoto hao 54 kila mmoja TZS. 45 Mil sawa na TZS. 2.43 Bil.
" Kama watoto hawa wangeenda nje ya nchi Serikali ingelipa TZS. 120 Mil kwa kila mtoto sawa na TZS. 6.5 Bil. hivyo kuokoa kiasi cha TZS. 4 Bil, "Amesema
Na kuongeza "Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali za umma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, " Amesema Dkt Mhavile
Aidha amesema Katika kukabiliana na tatizo la watoto la kutokusikia mwaka 2023, Serikari ilianzisha maabara ya kimataifa ya umahiri ya upasuaji na upandikizaji vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto na kuifanya kuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa na maabara hiyo.
"Hadi sasa madaktari wazawa 36 na wengine 18 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Nigeria, na Ghana pia wamepatiwa mafunzo kupitia maabara hiyo, " Amesema
Huduma ya Kibingwa Kupima Kiwango cha Kusikia Watoto Wachanga
Amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma ya ubingwa bobezi wa kupima watoto wachanga kiwango cha kusikia mara tu wanapozaliwa ili kugundua mapema na kutoa matibabu.
" Tangu kuanzishwa huduma hiyo mwishoni mwa 2023 tayari watoto wachanga 320 wamenufaika ambapo waliokutwa na changamoto hizo wako kwenye mpango maalum wa ufuatiliaji ikiwemo mafunzo ya kuongea na baadaye kupandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia, " Amesema Mhavile
Aidha Katika hatua nyingine Hospitali ya Muhimbili imeafanikiwa kuanzishwa Vipandikizi Meno (Dental Implant) .
"Tumeanzisha matibabu ya kuziba mapengo ambapo mzizi bandia hupandikizwa kwenye taya, kisha kuwekewa meno juu yake yanayogandishwa na kutumika kama sehemu ya meno yake ya kuzaliwa nayo," Amesema .
Pia Serikali imewezesha hospitali kununua mashine ya kisasa kabisa inayowezesha uchunguzi wa magonjwa ya mifupa ya taya pamoja na CT scan ya uso na kichwa kusaidia kupanga upandikizaji wa vipandikizi vya meno ambapo tangu kununuliwa mwishoni mwa mwaka 2024 tayari wagonjwa 2,251 wamenufaika.
0 Comments