NA AMINA SAIDI,TANGA.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga Uwasa imesema mahitaji ya Maji katika mji mdogo wa Muheza ni lita milioni 7.7 na yanayopatikana ni lita milioni 3.2 ikiwa ni pungufu ya mahitaji.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Kanda ya Muheza Ramadhan Nyambuka Ametoa taarifa hiyo alipokuwa akizungumza na Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji vilivyopo katika Mamlaka ya mji mdogo wa Muheza uliokuwa ukijadili mikakati ya kuondokana na tatizo sugu la uhaba wa maji wilayani hapa.
Amesema awali kabla ya Tanga Uwasa kukabidhiwa jukumu la kutoa huduma ya kusambaza maji mjini,Muheza katika kipindi cha kiangazi hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa ni chini ya asilimia 35 lakini sasa hivi imefikia asilimia 71.
Meneja huyo amesema kipindi hiki upatikanaji wa maji mjini Muheza ni mdogo kutokana na changamoto tatu Ambazo ni pamoja na ukame uliokausha chanzo kilichopo magoroto kukatika kwa umeme mara kwa mara na Ruwasa kuongeza maeneo kutoa huduma ya maji.
"Mgao wa maji uliopo kipindi hiki unatokana na changamoto ambazo ni kupungua maji kwenye chanzo cha Magoroto,tatizo la umeme kukatika mara kwa mara na Ruwasa imeongeza maeneo ya huduma ya maji" amesema Nyambuka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Muheza Kombo Dada amesema Madiwani na Wenyeviti watabeba jukumu la kutoa elimu kwa wakazi kuhusu utunzaji wa miundo mbinu,wizi wa Mita na wadaiwa sugu.
Diwani wa Kaya ya Masuguru Wilayani hapa Mohamed Bahoza ameitaka Tanga Uwasa kuongeza Kasi ya kufunga viungio vya maji mitaani ili kukabiliana na upoteaji wa maji.
Aidha Tanga Uwasa imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya kufikisha maji Muheza kutoa Moe jijini Tanga,Miji 28 ambayo itawezesha kuzalisha lita milioni 7.7 na lita za ziada zitakazohifadhiwa Kilulu kama akiba ya matumizi ya ziada.
0 Comments