Na Shomari Binda-Musoma Matukio Daima
VIJANA wawili kutoka jimbo la Musoma Vijijini wameibuka washindi wa kusoma na kuhifadhi Qur'aan yaliyofanyika leo machi 22,2025 kwenye ukumbi wa MCC mjini Musoma.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Kiislam Musoma mjini yalishirikisha vijana kutoka Wilaya za Bunda,Rorya,Butiama pamoja na Musoma mjini na vijijini.
Vijana hao walioshinda wanatoka kwenye madrasa ya Alhayatul Kariima iliyopo Kijiji cha Mkirira wakifundishwa na Ustadh Ismail Muhamed.
Kijana Abdurahi George ameshinda kwa kuwa mshindi wa kwanza kwa kuhifadhi juzuu moja na Musa Daud amekuwa mshindi wa kwanza kwa kuhifadhi juzuu 5 ambao wote wamepewa zawadi kwa ushindi huo.
Akizungumzia siri ya ushindi huo,mwalimu wa vijana hao Ustadh Ismail Muhamed amesema umakini na kushika mafundisho ndicho kilichowapa ushindi.
Amesema vijana wanapokuwa na utulivu kwenye madrasa na kumsikiliza mwalimiu ni rahisi kushika na kuhifadhi anachofundishwa.
" Niwashukuru vijana wangu wametuheshimisha Musoma vijijini kwa kushinda ushindi wa jumla kwa kuwa maeneo mengine yametoa mshindi mmoja mmoja.
" Niwashukuru umoja wa wanawake wa Kiislam Musoma mjini kwa kuandaa mashindano hayo na tunaomba watu mbalimbali kuwaunga mkono kwenye kazi nzuri wanayoifanya na ziwepo motisha za kutosha kwa vijana wanaofanya vizuri ili kuwahamasisha vijana wengine kusoma na kuijua dini.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma Ally Seif Mwendo alliyemwakilisha mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amewapongeza vijana hao kwa ushindi walioupata na kujifunza dini yao.
Amesema Qur'aan ni muongozo kama wanavyosema viongozi wa dini na ni vyema kuwaandaa vijana na kuwapeleka madrasa.
Mwendo amesema vijana wanapopata elimu ya dini wanakuwa na maadili mazuri na kuwapongeza umoja wa wanawake Musoma mjini kuandaa mashindano hayo kwa mwaka wa 5 mfululizo.
Mwenyekiti wa umoja huo Kalia Shomari Abadallah amesema licha ya kuandaa mashindano hayo kwa miaka 5 mfululizo zipo changamoto na kuomba ushirikiank kutoka kwenye ofisi ya mkuu wa Wilaya,taasisi za dini ya Kiislam na wadau mbalimbali.
Amesema licha ya kuandaa mashindano hayo moja ya jukumu lao ni kuifikia jamii na kutoa misaada ya kiutu kwa wenye uhitaji changamoto ikiwa ni kukosa miradi ya kiuchumi kupata fedha ya kutekeleza majukumu yao
0 Comments