Na Moses Ng’wat.Matukio Daima.
Uamuzi wa kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga SC na Simba SC, iliyokuwa ipigwe leo Machi 8, 2025, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ni pigo kwa soka la Tanzania.
Tukio hili linaacha maswali mazito kuhusu weledi wa uendeshaji wa ligi, uwajibikaji wa mamlaka husika, na hatma ya soka letu kwa ujumla.
Sababu za Kuahirishwa kwa Mechi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), mchezo huo umeahirishwa baada ya klabu ya Simba kudai kuzuiliwa kufanya mazoezi yao ya mwisho kwenye Uwanja wa Mkapa.
Hatua hii ilisababisha malalamiko kutoka kwa Simba, wakidai kuwa haki yao imevunjwa na taratibu za maandalizi ya mchezo hazikufuatwa ipasavyo.
TPLB imesema kuwa uamuzi huu umetokana na ripoti ya afisa usalama wa mchezo, ambayo imebaini kuwa kuna matukio yaliyohitaji uchunguzi wa kina.
Kwa sababu hiyo, bodi imeona ni busara kuahirisha mechi hiyo hadi pale hakikisho la usalama na usawa litakapothibitishwa.
Ukosefu wa Weledi katika Uendeshaji wa Ligi.
Uamuzi huu umeibua maswali mengi kuhusu weledi wa bodi ya ligi na mamlaka zinazohusika na uendeshaji wa ligi nchini.
Kwa ligi yenye hadhi kama NBC Premier League na inayoshika nafasi ya sita kwa ubora barani Afrika haikubaliki kuona mechi kubwa kama hii ikiingia katika sintofahamu inayozuia kuchezwa kwa wakati.
Maswali yanayojitokeza ni:
Kwa nini Simba ilizuiliwa kufanya mazoezi yao ya mwisho?
Je, kulikuwa na mawasiliano duni kati ya klabu husika na bodi ya ligi?
Ni nani anawajibika kwa sintofahamu hii?
Matukio haya yanaonyesha udhaifu katika usimamizi wa ligi na upendeleo wa wazi, ambao unahatarisha sifa ya soka la Tanzania kimataifa.
Tamko la Yanga na Maoni ya Mashabiki Baada ya kutangazwa kwa uamuzi wa kuahirisha mechi, msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amenukuliwa na mitandao ya kijamii akisema kuwa wao kama timu mwenyeji wa mchezo huo watapeleka timu uwanjani kama kawaida, kwani hawakufanya kosa lolote.
Hii inadhihirisha kuwa bado kuna utata mkubwa juu ya uamuzi huu na pengine bodi haikufanya tathmini ya kina kabla ya kufikia maamuzi.
Mashabiki kote nchini wanasemaje.
Kwa upande wa mashabiki, maoni yamegawanyika.
Ukipitia maoni mbalimbali ya mashabiki kutoka kona tofautitofauti kote nchini kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kumekuwa na mkinzano.
Wengine wanaunga mkono uamuzi wa bodi kwa msingi wa kuhakikisha haki inatendeka, huku wengine wakisema kuwa ni fedheha kwa soka letu na kitendo cha kuonesha kutokuwa na weledi katika uendeshaji wa ligi.
Hitimisho: Soka Letu Linakwenda Wapi?
Hili ni pigo kwa maendeleo ya soka la Tanzania.
Kwa mechi inayovutia mamilioni ya mashabiki ndani na nje ya nchi, TPLB ilipaswa kuwa na maandalizi thabiti ili kuepusha aibu kama hii.
Matukio kama haya yanaweza kupunguza hadhi ya ligi yetu na kuifanya isichukuliwe kwa uzito unaostahili kimataifa ikiwemo kuwa ligi namba sita kwa ubora Afrika.
Ni wakati sasa kwa viongozi wa soka Tanzania kujifunza kutokana na makosa haya, kuweka mifumo madhubuti ya kusimamia ligi, na kuhakikisha kuwa haki na usawa vinazingatiwa.
Kwa sasa, mashabiki wa soka wanasubiri tarehe mpya ya mchezo huu, huku wakibaki na maswali mengi bila majibu.
Je, tutaona mabadiliko, au hii itakuwa sehemu ya mzunguko wa migogoro isiyoisha kwenye soka letu?.
Mwisho.
0 Comments