NA SHAMILA RAJABU,MATUKIO DAIMA
Kutokana na wanawake wengi kukopa mikopo na kushindwa kurejesha na kujikuta wanaingia katika madhira ya kunyang'anywa mali zao walizoweka dhamana na taasisi mbali mbali za mikopo,Mhadhiri wa chuo kikuu cha Iringa Tuli Tweve amewashari akinamama kupata elimu ya fedha kabla ya kuchukua mikopo.
Tweve ameyasema hayo leo katika kipindi cha mwanamke kwanza kinachorushwa na Matukio Daima na kubainisha kuwa ukosefu wa elimu ya fedha huleta madhara kwa wanawake wanaokopa bila kuwa na matumizi sahihi ya fedha wanazokopa na kushindwa kurejesha kwa sababu fedha hizo haziendi kutumika katika kuingiza kipato.
Alisema kuwa wengi wao hujiingiza katika mikopo ya kausha damu yenye riba kubwa na kusababisha kushindwa kurejesha mikopo hiyo na kujikuta wanasambaratisha familia zao.
Ikiwa leo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani iliyobeba kauli mbiu ya ‘’Wanawake na Wasichana Tuimarishe Haki, Usawa, na Uwezeshaji” ambayo kitaifa yanafanyika Arusha huku Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
“Moja kati ya changamoto kubwa ambayo inawakumba wanawake kwa sasa ni suala la mikopo ya kausha damu na wengi wao hawana elimu ya kutosha kuhusiana na mikopo ya kausha damu hivyo hii inawafanya kuweza kujiingiza kwenye mikopo ambayo haizalishi matokeo yake mikopo inakuwa misiba kwenye familia zao kwasababu wengi wanachukua mikopo hiyo bila kuwa na malengo”
0 Comments