![]() |
Na Hamida Ramadhan, Matukio app Daima
MAMALAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imefanikiwa kuendelea kutoa huduma za Uchunguzi wa Kimaabara kwa Viwango vya Kimataifa kwa kufanikiwa kupata Ithibati ya umahiri wa uchunguzi wa kisayansi katika maabara zake.
Akizungumzia jijini Dodoma Mkemia Mkuu wa serikali Dk Fidelice Mafumiko wakati akielezea mafanikio na matarajio ya mamalaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk Samia amesema kuwa haya ni makubwa kwa GCLA na kwa Tanzania kwa ujumla, ambapo kwa sasa inao uwezo wa kupokea na kufanya uchunguzi wa sampuli na kutoa matokeo yanayokubalika kitaifa na kimataifa.
Amesema kuwa kukubalika huko kwa matokeo ya uchunguzi kunatokana na Mamlaka hiyo kutekeleza mifumo miwili ya ubora na umahiri ya kimataifa, ambayo ni Ithibati ya Mifumo ya Usimamizi wa Ubora (ISO 9001:2015), ya uendeshaji wa shughuli za GCLA uliyohuishwa kwa mara nne mfululizo na mfumo wa Ithibati katika Umahiri wa uchunguzi wa kimaabara (ISO17025:2027).
Dk.Mafumiko ameongeza kuwa uwekezaji katika mitambo na vifaa vya kisasa vya uchunguzi kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, imeiwezesha Mamlaka hiyo kununua mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma za uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara.
"Mitambo na vifaa hivi ni pamoja na mitambo mikubwa 16 na midogo 274 yenye thamani ya jumla ya Shilingi Bilioni 17.8. Ununuzi wa mitambo hii umeendelea kuimarisha uchunguzi wa kimaabara na kuendelea kutoa huduma bora za uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa wananchi kwa ufanisi zaidi," ameeleza Dk. Mafumiko.
Mkemia Mkuu huyo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk. Samia uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli,vielelezo umeongezeka kutoka sampuli 155,817 Mwaka fedha 2021/2022 hadi kufikia sampuli 188,362 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 21.
Dk. Mafumiko amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha huu wa 2024/2025,kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2024, sampuli 108,851 zilifanyiwa uchunguzi sawa na asilimia 104.50 ya lengo la kuchunguza sampuli 104,161.
Akizungumzia baadhi ya matarajio ya mamalaka hiyo inatarajia kuendelea kuimarisha huduma za Uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa sampuli na utoaji matokeo ya uchunguzi kwa wakati.
Amezitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na ununuzi wa mitambo ya uchunguzi ili kukabiliana na changamoto ya kukua na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuimarisha uchunguzi wa kimaabara na kuendelea kutoa huduma bora za uchunguzi wa Kisayansi wa kimaabara kwa wananchi kwa haraka na kwa wakati.
Dk. Mafumiko amesema nyingine ni kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo/umahiri watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi mkubwa kwa lengo la kuiwezesha Mamlaka kuongeza ubora wa utoaji huduma kwa wananchi, kutoa huduma za uchunguzi wa Kimaabara kwa kuzingatia Viwango vya Ubora vya Kimataifa.
Mwisho.
0 Comments