Header Ads Widget

AFUNGWA JELA MIAKA 20 KWA KUFUGA FISI NYUMBANI.



Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.


MAHAKAMA ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemuhukumu kifungo cha Miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31) maarufu kama Chief wa Kilulu kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya Fisi akiwa hai akiishi naye nyumbani kwake.


Mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilulu kilichopo Kata ya Bunhamala Wilayani Bariadi na Mganga wa kienyeji, alipewa adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa inamkabili kwenye Mahakama hiyo.


Hukumu hiyo imetolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo, Caroline Kiliwa mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.


Awali akisoma kosa la mshitakiwa, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mashtaka Mkoa Lupiana Mahenge alielezea Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo kosa lake ni kukutwa nyara ya serikali ambayo ni Fisi akiwa hai akimfuga nyumbani kwake kinyume cha sheria.


Alisema kuwa Januari 01, 2025 katika eneo la kijiji cha Kilulu mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema ambao walitoa taarifa kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani kwake.


Alieleza kuwa Mtuhumiwa aliishi na Fisi huyo kama mnyama wake wa kufuga kinyume na kinyume na kifungu cha 86 (1) kifungu kidongo na cha (2) (C) (III) cha sheria ya kuhifadhi wanyamapori sura ya 283 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Alisema kuwa kifungu hicho kinasomeka pamoja na haya ya 14, jedawali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya kupambana na uhujumu uchumi sura ya 200 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.


Upande wa mashitaka katika kuthibitisha kosa hilo ulipeleka mahakamani mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasina kuacha shaka.


Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne wakiwemo watoto mapacha ndipo Hakimu akatoa adhabu kwenda jela miaka 20 na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na watu wengine.


MWISHO.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI