Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, ameahidi kusaidia upatikanaji wa mkopo kwa mwekezaji mwenye ulemavu, Tunginie Sanga, anayemiliki shule ya awali na msingi ya Sanga T Forest katika eneo la Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.
Akizungumza wakati wa ziara yake shuleni hapo, Februari 26, 2025, Waziri Kikwete alibainisha kuwa dhamira ya Sanga katika kuboresha sekta ya elimu ni ya kupongezwa, hivyo serikali ina wajibu wa kumuunga mkono.
Aliagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbozi kuhakikisha mwekezaji huyo anapatiwa mkopo wa asilimia 10 wa halmashauri unaotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
"Nataka ifikapo Oktoba, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, tuone maendeleo makubwa katika mradi huu baada ya kupatiwa mkopo," alisema Waziri Kikwete.
Kwa upande wake, Sanga alisema tayari amewekeza shilingi milioni 79 katika ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, matundu matano ya vyoo na nyumba ya mwalimu.
Ameweka pia mkazo kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ya matunda, kivuli na maua.
Hata hivyo, alieleza changamoto anazokabiliana nazo na kusababisha kuomba mkopo ni ukosefu wa usafiri kwa wanafunzi, kutokuwepo kwa uzio wa shule, upungufu wa vyumba vya madarasa, na uhaba wa vifaa vya michezo kama bembea.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, alimpongeza Sanga kwa uwekezaji wake na kusisitiza kuwa elimu si biashara bali ni huduma muhimu kwa jamii.
Aliahidi kushughulikia haraka usajili wa shule hiyo ili kuwezesha upatikanaji wa mkopo na kuharakisha maendeleo yake.
Waziri Kikwete ambaye ni mlezi wa Mkoa wa Songwe kwa upande wa serikali alikuwa mkoani songwe kwa ziara ya siku tatu kwa kutembelea Halmashauri zote za Mkoa lengo likiwa ni kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.
Mwisho.










0 Comments