Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Abdulkadri Mushi (katikati) akikagua mradi wa ujenzi wa chumba cha upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti na njia za watembea wa miguu katika hospitali ya wilaya Kakonko akiwa kwenye ziara ya kamati ya siasa ya mkoa kukagua miradi
Na Fadhili Abdallah
Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Abdulkadri Mushi amemtaka Mkuu wa wilaya Kakonko na kamati ya siasa ya CCM ya wilaya hiyo kukemea na kuchukua hatua katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya wananchi ili kuifanya miradi hiyo kutekelezwa kwa viwango na kukamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi kunufaika na miradi hiyo.
Kadri alisema hayo katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo alipokuwa akiongoza kamati ya siasa ya mkoa Kigoma kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya wilaya hiyo na kusema kuwa miradi hiyo kutekelezwa kwa viwango na kwa wakati kuna faida kubwa katika kubadilisha maisha ya wananchi wa kawaida.
Alisema kuwa haiingii akilini kuona kuwa serikali inatoa fedha nyingi kutekeleza miradi ili kuleta maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wa kawaida lakini baadhi ya watu wanashindwa kusimamia au kwa maslahi yao wanafanya hujuma na miradi kushindwa kukidhi vigezo na kuchelewa kukamilika.
Katika wilaya hiyo mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya Taifa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ambayo kamati hiyo imetembelea ikiwemo shule mpya ya sekondari ya Ruhulu, Chuo cha VETA Kakonko, ujenzi wa maabara za sayansi katika shule ya wasichana Kakonko, ujenzi wa vibanda katika soko kuu la mjini Kakonko na miradi mitatu katika hospitali ya wilaya Kakonkoni.
Hata hivyo Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM alionyeshwa kusikitishwa na kutokamilika kwa mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya wilaya Kakonko ambao umesimama kwa miaka minane sasa baada ya fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kurudi hazina baada ya muda wa matumizi kupita bila kutumika hivyo kuahidi kulifanyia kazi suala hilo.
Awali katika miradi mbalimbali ambayo kamati hiyo imetembelea Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kakonko, Stephen Ndaki alisema kuwa miradi ya kimkakati ya Stendi ya mabasi ya Kakonko na soko kuu la wilaya hiyo ni miradi ya kimkakati ambayo inalenga kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema kuwa kukwama kulipwa kwa kiasi cha shilingi Zaidi ya milioni 500 kwa mkandarasi wa mradi huo kumesbabisha kushindwa kutekeleza malengo yao ya kutumia mradi huo kama chanzo kikubwa cha mapato na kwamba kwa sasa wanaendelea na jitihada za kuona mradi huo unapata fedha na kukamilika.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya Kakonko, Evance Mallasa alisema kuwa usimamizi madhubuti wanaoufanya umesaidia miradi mingi kukamilika kwa wakati na kuwa na viwango vilivyowekwa huku akibainisha kuwa taratibu za kimfumo na sheria za manunuzi kwa nyakati nyingine zimesababisha baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika jambo ambalo ni Zaidi ya uwezo wao.
0 Comments