Header Ads Widget

WANANCHI WAHIMIZWA KUDUMISHA NA KULINDA AMANI YA NCHI.


 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataka wananchi mkoani Mbeya na Tanzania kwa ujumla kudumisha na kulinda amani ya Taifa kwa kujiepusha na vitendo vya uhalifu kwani amani ndio chimbuko la maendeleo.

Kuzaga ambaye ni mlezi wa Kwaya ya Wasabato Mbeya Kati, ameeleza hayo Februari 07, 2025 wakati akizungumza na Wana kwaya wa Kanisa la Wasabato Mbeya Kati (Mbeya Adventist Church) wakiwa wanarekodi wimbo wao mpya unaozungumzia amani ya Afrika na Tanzania.

Kamanda Kuzaga amesisitiza umuhimu wa viongozi wa dini katika kukemea uovu na kuhubiri yaliyo mema ili kusababisha jamii kuendelea kubadilika kwa kuacha uhalifu na kuwa raia wema wakisaidia kudumisha amani nchini.




Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Mbeya Kati Christopher Mkama, amempongeza Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha amani ya nchi kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mwenyekiti wa Kwaya hiyo Peter Chacha, amewataka Watanzania kujifunza kupitia nchi nyingine zenye machafuko na kuwataka kuacha kuchezea amani kwani kwenye amani kunatoa fursa ya kuabudu na kufanya kazi za kujipatia kipato na kuendesha maisha kwa uhuru.

Naye Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa, amesema kuwa ipo nguvu kubwa ya kuzuia na kutokomeza uhalifu kupitia viongozi wa dini wakiwemo mapadri, mashekh na wachungaji kupitia mahubiri ya neno la Mungu.

Kwaya ya Kanisa la Wasabato Mbeya Kati kupitia wimbo wao "Amani" imewakumbusha wana Mbeya na Watanzania kwa ujumla kulinda na kudumisha amani ya Taifa kwa ujumla ambapo pamoja na wajibu huo wa waimbaji ni wajibu wa wenye mamlaka pia (viongozi) kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuwafanya watu kuipenda, kuiamini na kuifurahia nchi yao huku wakiendelea na majukumu yao bila kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI