Mapato ya ndani kuongezeka kwa asilimia 5.7
Na Moses Ng'wat,Tunduma.
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Wilayani Momba, limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 54.9 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayoub Mlimba, alibainisha Januari 30, 2025, kuwa makusanyo ya ndani yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 19.5, sawa na ongezeko la asilimia 5.7 kutoka bajeti ya mwaka uliopita.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha.
Alisema miongoni mwa vyanzo vilivyochangia ongezeko hilo ni kurejeshwa kwa chanzo cha maegesho ambacho awali ukusanyaji wake ulikuwa ukisimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), pamoja na ujio wa bandari kavu.
Pia, ushuru wa usafi wa mazingira kwa malori yanayopita kwenda nje ya nchi umesaidia kuongeza mapato.
Mlimba amesema chanzo hicho cha ushuru wa usafi wa mazingira kwa malori yanayopita kwenda nje ya nchi kinatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.5.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Innocent Maduhu, alisema asilimia 60 ya mapato ya ndani, sawa na shilingi bilioni 9.72, itaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, huku shilingi bilioni 1.6 zikitengwa kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
0 Comments