Na Moses Ng'wat, Ileje.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeleta madhara makubwa katika Shule ya Msingi Ilanga, kata ya Mlale, wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, na kusababisha paa la jengo la shule hiyo kuezuliwa huku wanafunzi 20 wakinusurika kifo.
Tukio hilo lilitokea Februari 11, 2025, majira ya mchana, wakati wanafunzi wakiwa darasani.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ostini Mdollo, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mvua hiyo ilisababisha uharibifu wa paa la vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya shule hiyo.
"Tunamshukuru Mungu hakuna vifo vilivyotokea, ingawa wanafunzi walipata hofu kubwa walipokuwa wakijaribu kujinusuru, huku wengine wakipata majeraha baada ya kuangukiwa na bati za paa," alisema Mdollo.
Kwa mujibu wa Mwalimu wa shule hiyo, Yusuph Tuya, shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 214 sasa imebakiwa na vyumba vitatu tu vya madarasa, hali inayolazimu wanafunzi kubadilishana muda wa kuhudhuria masomo.
Mwenyekiti wa shule hiyo, Said Mbisa, ameomba serikali na wadau wa maendeleo kusaidia kurejesha majengo yaliyoharibika ili wanafunzi waendelee na masomo yao bila hofu.
Diwani wa kata hiyo, Yotham Ndile, amesema mvua hiyo pia ilisababisha uharibifu wa nyumba za wananchi, mazao kama mahindi kuharibiwa vibaya, pamoja na kubomoka kwa kanisa moja.
Aidha, mwanafunzi mmoja kati ya 21 waliopata majeraha amepewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa matibabu zaidi.
Tayari wataalamu wa wilaya wamefika shuleni hapo kufanya tathmini na kushauri kuwa madarasa yaliyoathirika yajengwe upya kutokana na kutokuwa na ubora unaohitajika.
Shule ya Msingi Ilanga ilianzishwa mwaka 1980 kwa lengo la kupunguza safari ndefu ya wanafunzi waliokuwa wakitembea kilomita nane kufuata masomo katika Shule ya Msingi Mlale.
Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa miundombinu, shule hiyo sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya majengo, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi na walimu.
Mwisho.
0 Comments