Header Ads Widget

KAMPENI YA “VALENTINE WEEKEND GATEAWAY NA TANAPA” YAFANA WATALII 109 WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA KISIWA CHA SAANANE


Na Philipo Hassan - Mwanza


Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jana Februari 15 ilipokea takribani watalii 109 katika kilele cha Kampeni ya “Valentine Weekend Gateaway na TANAPA” iliyozinduliwa Januari 24, 2025 iliyolenga kuhamasisha watalii kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania  katika msimu wa Sikukuu ya wapendanao.


Watalii hao 109 iliwahusisha watalii wa ndani 98 na wengine 11 wakitoka nje ya mipaka ya Tanzania, wageni hao waliofika katika majira tofauti ambapo asubuhi waliingia watalii 60 na alasili walifika 49 miongoni mwao walilala katika mahema. Licha ya kutembelea vivutio mbalimbali nyakati za mchana pia walipata fursa ya kufurahia utalii wa usiku ikiwemo kuota moto usiku, safari za boti za usiku pamoja na utalii wa kuangalia nyota.


Akiwakaribisha Watalii hao Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dr. Tutindaga George, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, aliwapongeza watalii hao kwa kuchagua kutembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane wakati wa mchana na usiku, kwani nyakati za usiku jiji la Mwanza linamuoneka mzuri na kitofauti.


Aidha, Kamishna Dr. Tutindaga alisema, “Tunayo furaha kuwapokea leo hii, mmetutoa kimasomaso kwa kutembelea Hifadhi hii kwani mmehamasika vya kutosha na leo hii tumeona matunda ya uhamasishaji tulioufanya katika vyombo mbalimbali vya habari, ni matumaini yetu kama TANAPA kuwa mtafurahia urithi wenu na mtakaporudi katika maeneo yenu ya kazi mtakuwa mabalozi kuitangaza hifadhi hii na kuwaleta watanzania wengine nao waje wafurahie tunu hizi.”


Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo, anayesimamia Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA Makao Makuu, alielezea kuwa Kampeni ya Valentine “Weekend Gateaway na TANAPA” imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na watalii wengi kutembelea Hifadhi za Taifa, aidha kwa watalii waliotembelea Saanane wamefurahia utalii wa boti usiku “Night Boat Excursion”. Utalii huu wa boti usiku unakupa mwonekano na radha tofauti na utalii wa mchana kwani mandhari nzuri ya jiji la Mwanza na mwangaza wa stima ulioakisiwa na maji ya Ziwa victoria inakupa taswira isiyosahaulika maishani.”


Kamishna Jully aliongeza, “Wageni wamefurahi sana kutalii na boti usiku, kula chakula na vinywaji kwenye boti, kucheza muziki pamoja na kulala kwenye mahema ndani ya Hifadhi. Tunashukuru kwa huu muitikio uliopo na tunaamini aina hii ya utalii wa matukio utaendelea kukua na watanzania kuhamasika kuembelea Hifadhi za Taifa Tanzania.


TANAPA imeendelea kunadi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa nchini hasa kupitia matukio ambayo yanachangia hamasa ya watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa na kupelekea ongezeko la pato la Taifa pamoja na kukuza uchumi.











Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI