Na. Happiness Sam- Arusha
Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wakiongozwa na mwenyeji wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas jana tarehe 16, Februari 2025 walitembelea Hifadhi ya Taifa Arusha kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuunadi utalii wetu ndani na nje ya Tanzania.
Akiongea kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Abbas alieleza furaha yake ya kuwapokea viongozi hao, na kuwa uwepo wao katika Hifadhi ya Taifa Arusha ni chachu ya kupeleka ujumbe kwa Watanzania kutembelea maliasili hizo tulizorithishwa na waasisi wetu.
Dkt. Abbas alisema, “Viongozi hawa waandamizi wamekuja kufanya utalii na kujifunza. Kupitia uzoefu wa ziara hii watapata uelewa wa kina kuhusu usimamizi wa rasilimali na utunzaji wa mazingira, hivyo kuwa na mbinu bora zitakazosaidia kuboresha utendaji wao wa kazi.”
Naye, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed Said, alieleza kuwa kuwepo kwao ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha, kumewapa fursa ya kushuhudia makundi makubwa ya wanyamapori, mandhari ya kuvutia,maporomoko ya maji, na pia kutembelea eneo la kihistoria lenye mti mkubwa wa Mkuyu.
Mhandisi Zena alisema “Tumejifunza mengi na kuona vivutio vingi vya utalii. Tunashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuratibu safari hii kila tulipopita hapatasahaulika katika kumbukumbu zetu.”
Aidha, Viongozi hao pia, walitembelea maeneo mengine muhimu ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alifika kurekodi filamu ya “Amazing Tanzania”, ikionyesha vivutio vya utalii na urithi wa asili wa Taifa letu.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, alitoa shukrani kwa viongozi hao, kuchagua kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha kushuhudia vivutio mbalimbali vya utalii na maeneo ya kihistoria yanayopatikana ndani ya hifadhi hiyo kongwe nchini.
Kamishana Mwishawa alisema, “Tumefurahishwa na ujio wenu katika Hifadhi ya Taifa Arusha, hakika leo ni siku ya kihistoria ambapo viongozi wetu mmekuja kutembelea tunu hizi na kuunga mkono juhudi za Rais wetu kuitangaza hifadhi hii. Tunajivunia kuona Hifadhi ya Taifa Arusha ikizidi kuvutia wageni wengi zaidi”.
Katika kuhitimisha ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Malya ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha aliwashukuru Makatibu wakuu hao kwa niamba ya uongozi wa hifadhi na kuwaomba waendelee kuzitembelea Hifadhi za Taifa ili kutoa hamasa kwa watanzania wengine waliopo Bara na Visiwani kutembelalea maliasili zetu na kujifunza.
0 Comments