Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amewataka waombaji wa ajira serikalini kujiunga na mifumo ya Tehama ya serikali, ikiwemo Mifumo wa Ajira Portal.
Akizungumza jijini hapa,Waziri Simbachawene alisema kuwa hatua hii ni muhimu ili waombaji wapate taarifa sahihi na za haraka kuhusu nafasi za kazi zinazotangazwa na serikali. Alihimiza kuwa kujiunga na mifumo hii kutawasaidia waombaji kujisajili na kufuatilia maendeleo ya maombi yao kwa urahisi.
Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa uwazi na ufanisi katika mchakato wa ajira, akisema ni lazima waombaji wafuate miongozo na kutumia teknolojia ili kuongeza nafasi zao za kupata kazi.
Amekumbusha kwamba serikali inafanya juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza nafasi za ajira.
Aidha, amewataka vijana kujiandaa vizuri kwa ajili ya soko la ajira kupitia mafunzo na ujuzi wa kisasa, huku akiwashauri waombaji kuwa na subira katika kutafuta ajira, kwani serikali ina nia ya kutoa fursa zaidi kwa wananchi.
Waziri Simbachawene amefafanua kuwa Sekretarieti ya Ajira inatekeleza mchakato wa kuajiriwa kwa njia ya kidigitali kupitia "Ajira Portal", ambapo waombaji wanatuma maombi yao mtandaoni na kupata mrejesho wa papo hapo na Mchakato huu unajumuisha hatua tatu ambazo ni usaili wa kuandika, usaili wa vitendo, na usaili wa mahojiano.
Aidha, ametangaza kuwa kuanzia Januari 14 hadi Februari 24, 2025, usaili wa kada za Ualimu utafanyika nchini, ukilenga kujaza nafasi 14,648 ambapo Usaili huo utahusisha waombaji kufanya mtihani katika mikoa yao, hivyo kupunguza gharama za usafiri.
" Waombaji wanatakiwa kuhuisha taarifa zao katika Ajira Portal na kubeba vyeti vyao halisi siku ya usaili" Amesema
Waziri Simbachawene amesisitiza kuwa Sekretarieti ya Ajira inaendelea kushirikiana na Wizara mbalimbali na imeweza kuajiri watumishi wapya, hasa katika sekta ya afya, kwa mafanikio makubwa.
"Hivyo niwataka wote walioitwa kwenye usaili wa kada za Ualimu wajiandae vyema, kwani nafasi hizi ni za ushindani.
Aliongeza kuwa "Usaili huu utafanyika katika mikoa ya kila msailiwa ili kupunguza gharama za usafiri, na waombaji wanatakiwa kuhuisha taarifa zao katika Ajira Portal, hasa sehemu ya ‘current physical address, " Amesema
Waziri Simbachawene alikumbusha kuwa usaili wa awali wa kuandika (mchujo) utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono, kwa kada zote na ngazi zote za elimu.
Amesema waombaji wanatakiwa kubeba vyeti vyao halisi, ikiwa ni pamoja na Cheti cha Taaluma na Cheti cha Kuzaliwa, siku ya usaili.
0 Comments