Header Ads Widget

WATUMISHI WA MAHAKAMA SONGWE WAONYWA KUEPUKA UONEVU


Na Moses Ng'wat, Mbozi.

MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ameonya watumishi wa mahakama mkoani humo kuepuka vitendo vya uonevu, akisisitiza kuwa haki na usawa ni msingi muhimu katika kujenga jamii yenye amani.


Chongolo alitoa kauli hiyo, kupitia mwakilishi wake, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini, uliofanyika leo Januari 25, 2025, ambapo kimkoa, imefanyika katika viwanja vya Stendi ya Malori, mjini Vwawa, wilayani Mbozi.

Akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa katika hafla hiyo, Mgomi alisema kuwa watumishi wa mahakama wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu, wakizingatia misingi ya usawa, utawala bora, na haki kwa wote.

Aidha,  Mgomi aliwahimiza wananchi kuepuka kuchukua sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria katika kutafuta suluhisho la migogoro yao.


Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM, Mkoa wa Songwe, Radwell Mwampashi,akitoa salamu za chama hicho kwenye uzinduzi huo, amesisitiza umuhimu wa kuwafikia wananchi wa pembezoni ambao mara nyingi hawapati haki zao kutokana na kutokuwa na elimu juu ya mambo ya sheria.


Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Songwe, Francis Kishenyi, alisem kuwa,  wiki ya sheria ni fursa ya kipekee kwa mahakama kuzungumza na wadau wake kuhusu changamoto na mafanikio katika mfumo wa sheria.

Kauli mbiu ya Wiki ya Sheria mwaka huu, "Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,".

Katika maadhimisho hayo, taasisi za kisheria zitatoa huduma za bure za kisheria kwa wananchi kwa muda wa siku saba, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kisheria na ufumbuzi wa  matatizo.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI