Na: Zainab Ally - Dar es Salaam.
Makamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Viongozi Waandamizi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wameanza maandalizi ya safari maalum za treni kuelekea ndani ya Hifadhi ya Taifa Nyerere kwajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8, 2025.
Akiwa katika Stesheni za Reli hiyo kongwe nchini, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Jully Limo alisema, “Lengo la ziara hii na Makamishna wenzangu ni kufanya maandalizi kwani kwa taarifa tulizonazo kama taasisi mwitikio ni mkubwa na wanawake wengi wameonesha nia na hamu ya kushiriki safari hii kwa kutumia treni yenu ya TAZARA. Kwa mwaka jana safari hizi zilihusisha zaidi ya Wanawake 100 lakini kwa mwaka huu tunaweza ivunja hiyo rekodi ya mwaka jana.”
Aidha, Kamishna Jully pia aliambatana na Makamishna wengine kutoka Kanda ya Mashariki, Ofisi Kiunganishi ya Dar es Salaam, pamoja na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere - ACC Ephraimu Mwangomo ambaye atakuwa mwenyeji wa wageni hao watakapokuwa wakifanya utalii ndani ya hifadhi hiyo yenye vivutio vingi.
Ikumbukwe kuwa safari kama hizi zilifanyika pia mwaka jana 2024 ambapo zaidi ya wanawake 100 walitumia treni ya TAZARA, huku Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiingiza wanawake zaidi 1,000 Siku hiyo ya March 08, 2024. Hii ni hamasa kubwa iliyofanywa na wanawake wa kitanzania kwa kutembelea hifadhi tangu shirika hilo kuanzishwa mwaka 1959.
Kwa mwaka huu, TANAPA na TAZARA wanatarajia ongezeko kubwa la washiriki kutokana na maboresho ya huduma za usafiri wa reli na juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani, Treni hiyo itaelekea Hifadhi ya Taifa Nyerere, ambako wanawake watapata nafasi ya kushiriki katika shughuli za uhifadhi, kujifunza kuhusu maliasili, kufurahia mandhari ya Hifadhi,kuona Wanyamapori pamoja na aina mbalimbali za ndege.
0 Comments