Header Ads Widget

MSEMAJI - MSIGWA AWAPONGEZA TANAPA KWA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UHIFADHI




Na: Zainab Ally - Mikumi


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuimarisha matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi, hatua inayolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato, utangazaji wa utalii, na kukuza fursa za uwekezaji ili kuongeza mazao ya utalii na mapato kwa Taifa.


Akizungumza jana, Januari 25, 2025, katika mkutano na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dodoma na Morogoro uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Msigwa amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa  Tanzania (TANAPA) kwa matumizi ya sayansi na teknolojia katika Uhifadhi wa maliasili ili ziendelee kuwepo kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Alisema, “Shirika letu la TANAPA limeendelea kuongeza jitihada za matumizi ya sayansi na teknolojia katika kulinda rasilimali za taifa. Unapozungumzia uhifadhi, ni pamoja na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa kwa askari wanakuwa porini wakifanya doria, vifaa hivyo ni pamoja na GPS, matumizi ya ndege nyuki kusaka na kuonyesha walipo majangili pamoja na intelijensia ya kuwajua jangili walipo na wanapanga nini kabla hawajaleta madhara na uharibifu hifadhini.


Aidha, Msigwa alitanabaisha kuwa TANAPA imeendelea kupunguza migogoro baina ya wanyamapori waharibifu na hatarishi kwa binadamu kwa kuwafunga viongozi wao Visukuma mawimbi (GPS Collars) ili kujua makundi hayo ya tembo yana uelekeo gani kwa minajili ya kuzuia madhara ya kuibukia katika vijiji vya jirani na kuleta taharuki.


“Vilevile, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefunga kamera za kisasa katika maeneo mbalimbali ili kufuatilia mienendo ya wanyamapori adimu na walio hatarini kutoweka kama Faru, Sokwe, na Mbwa Mwitu ili kujua wanachunga maeneo gani na nini kinawasibu kwa wakati huo wawapo malishoni”, aliongeza Msemaji huyo.


Sambamba na hilo pia, Msigwa alilipongeza Shirika hilo la Uhifadhi Endelevu kwa ubunifu wa kuanzisha mazao mapya ya utalii. Alisema kuwa hatua hiyo imeongeza idadi ya watalii kufikia 1,863,108 kwa mwaka 2023-2024 kutoka 1,618,538 kwa mwaka 2022-2023, ongezeko la asilimia 15.


Kufuatia mikakati hiyo Serikali kupitia TANAPA tayari imeanza kaleta matunda, ambapo mwaka wa fedha 2024-2025 walitarajia kukusanya shilingi bilioni 430.9 lakini hadi kufikia Juni 2024, TANAPA ilikuwa imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 325.1 hali inayoleta taswira chanya ya kuvuka malengo walijiweka ifikapo  June 30, 2025.


“Makadirio yetu ni bilioni 430, lakini kwa kasi mliyonayo, mnaweza kuvuka malengo, hatua ambayo itavunja rekodi,” aliongeza Msigwa.


Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Augustino Massesa, alisema mafanikio ya ukusanyaji mapato yanatokana na jitihada za kuboresha miundombinu, kuongeza vyumba vya kulala wageni, na kutoa huduma bora kwa watalii, zikiwemo safari za karibu za kuona wanyama.


Hatua za Serikali, kama matumizi ya teknolojia, ubunifu wa bidhaa za utalii, na kampeni za kimataifa kama Royal Tour, zimeifanya sekta ya utalii kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa, ikichangia ajira na maendeleo ya kijamii kwa ujumla.













Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI