Na Lilian Kasenene,Morogoro
WANANCHI wa Kata ya Magomeni Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wameondokana na athari za mafuriko pindi mto Mkondoa unapojaa maji baada ya kujengewa mfereji wa maji ya mvua wa mita 1,800 na vivuko vinne na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF.
Kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini unaosimamiwa na mfuko wa TASAF umewafikia wananchi hao kwa kujenga kuta na kitako kwenye mfereji huo ili usimomonyoke.
Mradi huo uliogharimu sh milioni 64.56 zikiwemo milioni 47.8 za ujira kwa walengwa na milioni 16.8 za ununuzi wa vifaa, usimamizi na ufuatiliaji uliojengwa kipindi cha pili cha utekelezaji wa TASAF uliohusisha ufukuaji wa mtaro, ujenzi wa vivuko vinne.
Risala ya wananchi iliyosomwa mbele ya viongozi wa TASAF Makao makuu, wadau wa maendeleo kutoka benki ya Dunia,Ubalozi wa Uswis,Ireland, Norway, na wadau wengine wanaochangia mfuko wa TASAF pamoja na viongozi wa Serikali, Msimamizi wa walengwa wa TASAF kata ya Magomeni Tatu Daudi alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huo Kijiji Cha Rose na vingine vya jirani ikiwemo Mbwamaji na Kiyangayanga vilikuwa na changamoto ya mafuriko hasa wakati wa mvua.
"Kwa kipindi kîefu maji yalikuwa yakikosa uelekeo na kujaa kwenye makazi na nyumba nyingi zilikuwa zikiathiriwa na maji, lakini pia magonjwa kama malaria na Kuhara kutokana na maji kutuama ovyo na yalikuwa ni changamoto kubwa kwetu,"alisema Tatu.
Alisema baada ya utekelezaji wa mradi huo, makazi ya wananchi sasa yameokolewa na kuwa salama, na hakuna athari za mafuriko Tena,magonjwa yanayosababishwa na maji kutuama yamekwisha huku wananchi wakiishi bila shaka hasa wakati huu wa mvua.
Aidha akasema kupitia utekelezaji wa mradi huo, walengwa wamepata ujuzi na stadi mbalimbali katika upandaji wa nyasi za uhifadhi wa mazingira, ujenzi wa kutumia mawe, namna ya kuchimba mifereji na ujenzi wa mifereji sambamba na walengwa kujiongezea kipato kutoka 24,000 kufikia 30,000.
Kuhusu changamoto zilizojitokeza wakati wa mradi alisema ni pamoja na uchache wa Fedha za vifaa wanazotengewa kwani hadi sasa mfereji huo imejengwa kwa mita 427 tu kwa mawe na kutishia sehemu nyingine iliyobaki kukabiliwa na mmomonyoko na kuzalisha mto katikati ya makazi.
Mratibu wa TASAF wilaya ya Kilosa Dedan Mauhe,alisema kwa upande wa Kilosa waliwatambua walengwa 6,049.wa zamani sawa na asilimia 70 na wapya 4,566 sawa na asilimia 30 na kufanya walengwa wote katika Halmashauri ya wilaya hiyo kufikia 10,615.
Hata hivyo akasema hadi sasa kuna jumla ya walengwa 8,899 baada ya wengine kuhitimu na kuondoka kwenye kundi la walengwa baada ya kufanikiwa, kufariki dunia kuhama maeneo bila taarifa ama sababu nyinginezo.
Akasema katika kipindi cha Julai hadi Agosti 2020 hadi Septemba-Oktoba 2024 walipofungua dirisha waliweza kulipa zaidi ya sh bilioni 8 kama Fedha taslimu kwa wanufaika kwenye vijiji 159 na bilioni 1.4 kwa njia ya mitandao ya kielektroniki ya simu ama benki.
Naye mratibu wa TASAF mkoa wa Morogoro Jacob Kayange alisema jumla ya shilingi bilioni 60.3 zimetolewa kwa walengwa 42,607 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 katika mkoa wa Morogoro.
Kayange akasema kwa kipindi hicho sh miioni 783.8 zimechangwa na vikundi 3,221 vinavyohusisha walengwa 36,182 katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro ambapo miongoni mwao Wanawake ni 30,458 na wanaume ni 5,719.
Kwenye Ruzuku za uzalishaji akasema kiasi cha sh bilioni 1.7 zimetolewa kwa walengwa 4,807 kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya uzalishaji.
Katika kipindi hicho pia kupitia kaya, vijana 122 wamenufaika kwa kujiunga na vyuo vikuu, 81 vyuo vya kati, ukakika wa watoto wa umri wa chini ya Miaka mitano kuhudhuria kliniki na wale wa zaidi ya Miaka mitano kuhudhuria shule kikamilifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa miradi kutoka TASAF makao makuu John Elisha akasema lengo la tukio wa Timu hiyo ya wafadhili na viongozi wa TASAF Makao makuu ni kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba timu zaidi ya tatu zinazunguka maeneo mbalimbali nchini kuona hali hiyo na kuzungumza na wananchi.
0 Comments