Na Matukio Daima media
MJUMBE wa mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Wilaya ya Iringa Vijijini,Festo Kiswaga, amepongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyotolewa tarehe 31 Desemba 2024 imeonesha Jinsi Taifa lilivyopiga hatua kubwa chini ya uongozi wake.
Alisema kuwa katika hotuba hiyo, iliyokuwa na imelenga kuhitimisha mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025, ilibeba maudhui mbalimbali yanayohusu maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa ya Taifa letu.
Alisema kuwa katika hotuba yake, Rais Samia alitathmini mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka 2024, changamoto zilizokabiliwa, na mipango ya Serikali kwa mwaka 2025. Hotuba hiyo ilijikita katika kuimarisha uchumi wa Taifa, kuendeleza huduma za kijamii, na kukuza ustawi wa wananchi.
Kiswaga ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Monduli mkoani Arusha katika mahojiano yake na Matukio Daima Tv jana alipongeza maono ya Rais Samia na uwezo wake wa kuongoza nchi kwa hekima na weledi kuwa mafanikio yaliyopatikana mwaka 2024 ni ushahidi wa jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia.
Hivyo aliipongeza Serikali kwa kufanikisha ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.4, ongezeko la uwekezaji wa Dola za Kimarekani bilioni 7.7, na usimamizi thabiti wa deni la Taifa.
Pia alisisitiza kuwa juhudi za Serikali katika sekta za kilimo, elimu, afya, na miundombinu zinaimarisha maisha ya wananchi wa kawaida.
Kiswaga aliongeza kuwa mwaka 2024 ulikuwa wa kihistoria kwa Tanzania, kwani Taifa liliadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano, na umoja wa kitaifa.
Hivyo Kiswaga alibainisha kuwa hotuba ya Rais iliwakumbusha wananchi umuhimu wa kuenzi misingi ya Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Kiswaga, maadhimisho hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa na yalionesha uwezo wa Tanzania kuwa nchi yenye mshikamano wa kijamii na kisiasa. Alipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kulinda amani ya nchi, huku akiwashukuru wananchi kwa kudumisha utulivu.
Mjumbe huyo wa CCM alielezea kuridhika kwake na mageuzi yaliyofanyika katika mfumo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo wagombea walihitajika kupata ridhaa ya wananchi hata kama walikuwa hawana wapinzani. Alisema kuwa mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kukuza demokrasia nchini.
Kwani alisema hotuba ya Rais Samia ilibainisha mafanikio makubwa ya kiuchumi, ikiwemo ongezeko la mapato ya Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo ilikusanya shilingi trilioni 21.276 kati ya Januari na Oktoba 2024.
Kiswaga alisema kuwa ongezeko hili ni matokeo ya sera bora za kifedha na usimamizi wa rasilimali za nchi.
Hata hivyo alisifu juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya uwekezaji, ambapo miradi 865 ilisajiliwa, na miradi mikubwa ya viwanda ilianzishwa chini ya Mamlaka ya EPZA.
Akielezea matumaini yake kwamba uwekezaji huu utaongeza ajira kwa vijana na kukuza ustawi wa jamii Kiswaga aliipongeza Serikali kwa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia, hususan kupitia ziara za Rais Samia katika nchi mbalimbali kama Korea Kusini na China.
"Ziara hizi zilichangia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupata misaada ya kifedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mfano, Rais Samia alifanikiwa kupata Dola za Kimarekani bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini kwa ajili ya miradi ya miundombinu, elimu, na afya alisisitiza kuwa mafanikio haya yanaonyesha umahiri wa Rais Samia katika kuendesha diplomasia yenye tija kwa Taifa"
Mjumbe huyo alielezea kufurahishwa na maendeleo ya miradi ya kimkakati kama Bwawa la Umeme la Julius Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR). Alisema kuwa miradi hii ni mifano hai ya jitihada za Rais Samia kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, alitaja juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya anga kupitia ununuzi wa ndege mpya na kuimarisha viwanja vya ndege, akisema kuwa hatua hizi zitasaidia kuimarisha utalii na biashara nchini.
Pamoja na mafanikio hayo, Kiswaga alibainisha kuwa mwaka 2024 ulikuwa na changamoto zake, ikiwemo athari za mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya, pamoja na upungufu wa fedha za kigeni. Hata hivyo, alisifia jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo kupitia mipango na mikakati madhubuti.
Festo Kiswaga alielezea matumaini yake na watanzania kuwa mwaka 2025 utakuwa wa mafanikio zaidi, kwa kuzingatia mipango ya maendeleo iliyowekwa na Serikali. Alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi zake za kuimarisha ustawi wa Taifa.
Alisema kuwa hotuba ya Rais Samia ni mfano wa uongozi thabiti na wenye maono. Alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, mshikamano, na juhudi za kujiletea maendeleo na wajibu wa watanzania kuendelea kumuunga mkono zaidi.
0 Comments