Na Gabriel kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Jeshi la Polisi Wilayani Njombe limewaonya vijana kutojihusisha na vitendo vya uvutaji dawa za kulevya,Uchezaji kamali na kujiingiza kwenye magenge hatarishi yanayoweza kuwasababishia madhara ya kiakili na kimwili kwani Taifa linawategemea.
Onyo Hilo limetolewa na Afande Andrew Choyo kwa niaba ya mkuu wa Polisi wilaya ya Njombe wakati wa uzinduzi wa Filamu ya KIPAJI PART ONE ya msaani George Kalenge maarufu kwa jina la Sharobaro wa Njombe iliyobeba maudhui ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya ambapo Amesema mbali na madhara mengi ya matumizi ya dawa za kulevya lakini Sheria zitachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na matumizi ya dawa hizo.
Mgeni wa Heshima katika uzinduzi wa Filamu hiyo ni Baraka Ndandu Mfanyabiashara akiwakilishwa na Salumu Mohamed Katibu wa Taasisi ya sanaa Njombe ( Tasunjo) yeye anawataka vijana kushikana katika kazi zao huku wakitakiwa kuandaa Maudhui yanayozingatia tamaduni na Mila za kiafrika ili jamii nzima iweze kunufaika.
Clemence Manga ni Ofisa Utamaduni na Michezo halmashauri ya Mji Njombe ambaye anawasisitiza wasanii kusajili kazi zao Basata ili waweze kutambulika na serikali kwani itakuwa rahisi kusaidika kama ilivyo kwa Sharobaro wa Njombe.
Akiwashukuru wadau mbalimbali waliofika kushuhudia uzinduzi wa Filamu hiyo Msanii George Kalenga(SHAROBARO WA NJOMBE) ameitaka jamii kujifunza maudhui yaliyomo kwenye Filamu hiyo inayotoa elimu ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya na kwamba yeye pia hatumii tofauti na jamii inavyomuona kupitia sanaa.
Hata hivyo kupitia sanaa ya uigizaji sauti umetolewa ujumbe na Msanii ''Baraka Magufuli'' akitaka vijana kuwa wazalendo katika Taifa lao kwa kufanya sanaa zinazoweza kuibadilisha jamii kwa mtazamo chanya wenye mrengo wa kuliletea Taifa Maendeleo.
0 Comments