Header Ads Widget

UVCCM IRINGA WATEMBELEA HIFADHI YA RUAHA

 


Zaidi ya watalii wa ndani 33 kutoka Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wakiongozwa na Emmanuel Ngabuji ambaye ni Afisa Tarafa wa Pawaga wilayani Iringa wametembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hii ya pili kwa ukubwa Tanzania ikiwa na eneo la kilometa za mraba 19,822.


Wakiwa ndani ya hifadhi hiyo Vijana hao wamejionea vivutio mbalimbali wakiwemo wanyamapori mbalimbali kama vile Tembo, Nyati, Pundamilia, Kudu na Swala huku wakishuhudia uboreshwaji wa miundombinu ikiwemo malazi, viwanja vya Ndege na barabara.


Aidha, Afisa Tarafa Ngabuji alisema, “Licha ya kuvutiwa na mandhari nzuri, wanyama na ndege wa aina tofauti tunaahidi kuwa mabalozi wa kuvinadi vivutio hivi na kuwahamasisha watanzania wenzetu kuja kutembelea hifadhi hii hasa kipindi hiki cha Msimu wa sikukuu za Mwisho wa mwaka kwani ndio muda mzuri wa kuungana na familia zetu na kufurahia urithi maridhawa tuliachiwa na viongozi wetu.”


Naye, Afisa Mhifadhi Mkuu Faustine Sabato, kwa niaba ya Mkuu wa hifadhi hiyo aliwataka vijana hao wa Chama Tawala kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ujangili vinavyorudisha nyuma jitihada za Uhifadhi nchini na kulisababishia Taifa kukosa mapato yanayotokana na utalii kama vitendo vya ujangili havitadhibitiwa.


Ziara hiyo ya Vijana hao wa Umoja wa Vijana wa CCM wilaya ya Iringa vijijini ilifanyika jana Desemba 22, 2024 ikiwahusisha Mwenyekiti na Katibu wa Umoja huo, Afisa tarafa, afisa mahusiano na wajumbe wengine wa CCM huku mkazo ukisisitizwa kwenye ulinzi wa maliasili hizo ili zitumike sasa na kwa vizazi vijavyo.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI